SERIKALI imetoa ufafanuzi kuhusu tatizo la
ajira nchini, huku wanasiasa
waliozungumzia tatizo hilo kuwa ni bomu,
wakitakiwa kutoa ushauri wa namna ya
kulitegua au kupunguza athari zake kama
likilipuka.
Mbali na ushauri huo, Serikali pia
imewataka wanasiasa wanaotumia tatizo
hilo kisiasa, kuonesha mfano wa kusaidia
vijana katika majimbo yao kwanza, badala
ya kusubiri siku wakipewa nchi.
Mawaziri wanne walitumia muda wao jana
kujibu hoja hiyo, ambayo ni hoja lulu

kisiasa, kutokana na hali halisi kuwa
sehemu kubwa ya Watanzania ni vijana,
hivyo inatazamwa na wanasiasa wengi
kuwa ndio watakuwa sehemu kubwa ya
wapiga kura.
Kutokana na umuhimu wa ajira katika siasa
za leo, Naibu Spika, Job Ndugai hivi karibuni
alisema Mtanzania mwenye nia ya
kugombea urais mwaka 2015, ili aeleweke
kwa wananchi, ni lazima aeleze mikakati ya
kuwasaidia vijana kupata ajira.
"Ajira ni tatizo kubwa na lazima
lishughulikiwe. Kuna vijana hawaendi shule,
lazima watazamwe. Kuna wanaomaliza
darasa la saba, kidato cha nne, cha sita na
vyuo vikuu.
"Nazungumza kutoka moyoni kabisa. Hizi ni
dakika za mwisho za 
Serikali ya Awamu ya
Nne, wale wanaojipanga kwa Awamu ya
Tano kama hawataongelea ajira, basi
waandike wameumia," alisema Ndugai.
Alianza Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia
Kabaka, ambaye alikiri kuwa ajira ni tatizo,
lakini akafafanua kuwa si la Tanzania tu,
bali pia ni tatizo la kimataifa.
Alisema katika utafiti uliofanyika mwaka
2012, ilionekana ajira ya muda mrefu,
inayompa mwajiriwa hifadhi kuwa
imeongezeka kwa asilimia 13.5. Ongezeko
hilo limetolewa katika sekta ya umma,
ambayo imetoa asilimia 35.8 ya ajira huku
sekta binafsi ikitoa asilimia 64.2 ya ajira.
Kutokana na mchango mkubwa wa sekta
binafsi katika ajira, Kabaka alisema Serikali
imekuwa ikiweka mazingira rafiki kwa
wawekezaji, ikiwemo ujenzi wa barabara,
kuboresha upatikanaji wa nishati ya
umeme na mawasiliano.
Alisema wakati wanasiasa wanasema
Tanzania kuna tatizo kubwa la ajira, ambalo
kitakwimu ni asilimia 11.7, nchini Afrika
Kusini ni asilimia 24.9.
"Sasa kabla ya kusema ukipewa nchi utatoa
ajira, tuoneshe kwanza katika jimbo lako.
Umefanyaje kuongeza ajira katika sekta
isiyo rasmi…msidanganye wananchi na
kuwachonganisha na Serikali," alisema.
Kuhusu fursa ya kufanya mafunzo kwa
vitendo, Serikali imezungumza na Chama
cha Waajiri (ATE) ili watoe fursa hizo kwa
wanafunzi wanaotoka katika vyuo
mbalimbali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Asiye na Wizara
Maalumu, Profesa Mark Mwandosya,
aliamua kuonesha mfano kwa kuanza
kutoa ushauri.
Alitoa hatua kumi, alizotaka waajiriwa
watarajiwa walio katika soko ambao
hawajapata ajira na walio vyuoni na
wanaojiandaa kujiunga na vyuo mbalimbali,
ili wapate ajira.
Kwanza aliwataka wanafunzi wanaojiunga
na vyuo, kama wanataka kuajiriwa,
wachukue fani za sayansi, teknolojia na
uhandisi.
Pili, aliwataka wanaosomea  uhandisi na
sayansi, wachanganye fani hiyo na fani ya
usimamizi wa biashara.
Tatu, aliwataka wanaochukua fani za sanaa,
pia kuchukua fani za usimamizi, kwa maana
ya Shahada ya Uzamili ya Usimamizi (MBA).
Profesa Mwandosya pia aliwataka
waajiriwa watarajiwa, wasidharau lugha za
Kiswahili na Kiingereza ;na wazizungumze
kwa ufasaha, lakini akawataka pia
kuchukua lugha moja katika ya Kifaransa,
Kihispania, Kireno na Kichina.
Hatua nyingine waliyoshauriwa kuchukua
ni kutoogopa kushindana katika soka la nje,
ikiwemo soko la Afrika Mashariki, Afrika na
sehemu nyingine duniani. Kwa mujibu wa
Profesa Mwandosya, katika soko hilo la ajira
kuna Wakenya, Warwanda na Waganda.
Aliwataka wanafunzi vyuoni kuanza
kujijengea kichwani dhana ya kujiajiri, kwa
kuwa ni jambo zuri ili wasingoje kupata
ajira za Serikali.
Wasomi hao pia walitakiwa waache
kuchagua kazi wala ngazi ya kuanzia kazi,
kwa kuwa hata aliyesomea uhandisi
akianzia kazi ya fundi mchundo, atapanda
haraka. Pia, aliwataka wajiamini, wawe
wabunifu na kujiunga katika vikundi ili
wawezeshwe.
Credit: Habari Leo
 
Top