Suarez amesema kuna baadhi ya mambo ambayo hutokea uwanjani na hayapaswi kuzua kashfa
Shirikisho la soka duniani limeanzisha uchunguzi dhidi ya mchezaji wa Uruguay Luis Suarez, baada ya kuonekana akimng’ata mchezaji wa Italia, Giorgio Chiellini wakati wa mechi yao ya kombe la dunia.
Suarez ambaye pia huchezea Liverpool katika ligi ya Uingereza pamoja na shirikisho la soka la Uruguay wana hadi leo kujibu FIFA.

Suarez, aligongana na Chiellini wakati wa mechi yao Jumanne usiku katika awamu ya mtimuano, ambapo Uruguay ilishinda bao moja bila dhidi ya Italia.
Refari wa mechi hiyo hakuchukua hatua yoyote dhidi ya Suarez.
Ikiwa atapatikana na hatia, Suarez huenda akazuiwa kucheza mechi 24 au kwa miaka miwili.
Suarez mwenyewe tayari amejitetea katika vyombo vya habari nchini Uruguay
"Kuna mambo ambayo hutokea uwanjani,’’ alisema Suarez. “Tuligongana , yeye aligonga kwa bega lake katika sehemu ya mdomo.’’
Chiellini alishusha jezi lake kuonyesha sehemu aliyong’atwa katika bega lake.
"Kuna mambo fulani ambayo hutokea uwanjani na sidhani ni vyema kuanza kuzua kashfa kutokana na mambo kama hayo. Yanapaswa tu kuishia uwanjani,’’ alinukuliwa akisema Suarez.
Chiellini, mwenye umri wa miaka 29, alisema angependa kuona ikiwa FIFA wana ujasiri wa kutumia ushahidi wa video kumuadhibu Suarez, kwa sababu refari aliona lakini hakuchukua hatua.

Tukio hilo lilifanyika kuelekea mwishoni mwa mechi , muda ,mfupi kabla ya Uruguay kuingiza bao la ushindi kwenye mechi hiyo dhidi ya Italia.
 
Top