Mwanafunzi wa kike wa darasa la saba anayesoma katika Shule ya Msingi Chanzige B iliyopo Kisarawe, Pwani aliyefanyiwa unyama wa kulawitiwa na vijana watatu.
Denti mmoja wa kike wa darasa la saba anayesoma katika Shule ya Msingi Chanzige B iliyopo Kisarawe, Pwani amejikuta katika wakati mgumu baada ya kulawitiwa na kusababishiwa maumivu makali sehemu zake za siri.
Simulizi ya binti huyo inayouma sana, inaeleza kuwa denti huyo alifanyiwa unyama huo na vijana watatu ambao bado hawajafahamika majina yao mara moja lakini amekuwa akimtaja mmoja kwa jina la Musa.
Tukio hilo lenye sura ya majonzi hasa kwa wazazi na watoto, lilitokea hivi karibuni Kisarawe mkoani Pwani lakini ilifanywa siri kwa muda mrefu na mtoto huyo kukaa bila matibabu.
Chanzo chetu cha habari kinasema kuwa, shangazi wa mtoto huyo ambaye anaishi naye ndiye sababu ya kutopata tiba, kwani anadaiwa kuchukua kiasi cha shilingi 200,000 kutoka Musa anayetajwa kuwa mmoja wa wahusika kama kifunga mdomo.
Chanzo hicho kikazidi kusema kuwa, awali kesi hiyo ilifikishwa katika Kituo cha Polisi Kisarawe na kufunguliwa jalada lakini shangazi wa mtoto huyo aliamua kuyamaliza mambo hayo na mmoja wa watuhumiwa baada ya kupewa kiasi hicho cha fedha.
Uchunguzi wa Amani umegundua kuwa, sakata hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi Kisarawe na kufunguliwa jalada nambari KIS/RB/326/2014, ambapo Fomu ya Polisi Nambari 3 (PF3) ilitolewa kwa ajili ya matibabu ya mtoto huyo.
Akisimulia zaidi, mama mzazi wa mwanafunzi aitwaye Mariam Said alisema, alipata taarifa za mwanaye kukumbwa na masahibu hayo ambapo aliamua kusafiri kutoka Mlandizi anapoishi hadi Kisarawe kufuatilia tukio hilo.
Binti huyo alisema alifanyiwa ukatili huo wakati akitokea shuleni na kwamba alimweleza shangazi yake kila kitu kuhusiana na tukio hilo kabla ya kwenda naye polisi kutoa taarifa.
“Baada ya hapo tulikwenda katika Hospitali ya Kisarawe lakini sikupata matibabu kwa sababu shangazi alisema hana pesa ya malipo, kukarudi nyumbani na kununua dawa kwenye maduka ya dawa,’’ alisema mtoto huyo na kuongeza:
“Pale hospitalini, shangazi alitakiwa kutoa kadi ya Bima au shilingi 10,000 ili nitibiwe. Sasa hakuwa na Bima wala hiyo pesa ndiyo maana ikashindikana.”
Gazeti hili lilifunga safari hadi Shule ya Msingi Chanzige B na kuzungumza na Mwalimu Mkuu, Issac Eliah ambaye alikiri kupokea taarifa ya mwanafunzi wake kubakwa na kulawitiwa kutoka kwa shangazi wa mtoto huyo na kutoa ruhusa kwa ajili ya matibabu.
Shangazi wa mtoto huyo alipotakiwa kuzungumzia ishu ya kuzima kesi hiyo kwa madai ya kupewa shilingi 200,000 alisema: “Mimi sitaki kuzungumzia suala hilo, nendeni polisi mkaulize siyo kuniuliza mimi.”