Wananchi wa kata ya Magara katika wilaya ya Babati mkoani Manyara, wamelalamikia ukosefu wa daraja katika mto magara, licha ya ahadi za mara kwa mara za kujenga daraja zilizotolewa na wagombea uraisi wa vyama mbalimbali hali inayosababisha wanafunzi kusoma wakati wa kiangazi pekee kutokana na wakati wa masika mto kujaa maji na wananchi na wanafunzi kushindwa kuvuka upande wa pili kufuatia mto huo kujaa na hivyo kutoruhusu magari na watu kuvuka.
Wananchi hao wamesema, ukosefu wa daraja katika eneo hilo, unakwamisha kwa kiasi kikubwa shughuli za maendeleo na wakati mwingine husababisha maafa na hasara kutokana na watu na magari kusombwa na maji huku wanafunzi na wagonjwa wakishindwa kupata huduma kutokana na kutokuwepo kwa uwezekano wa kuvuka upande wa pili ambapo wameiomba serikali kujenga daraja katika mto huo ili kuharakisha maendeleo.
Kwa upande wake mkuu wa idara ya ujirani mwema katika hifadhi ya taifa ya ziwa manyara Ibrahim Ninga amesema ukosefu wa daraja katika mto huo unaopeleka maji yake katika ziwa manyara ni kikwazo kwa sekta ya utalii kutokana na watalii kutoweza kuitumia barabara hiyo na kwamba kutokana na tatizo hilo hifadhi ya ziwa manyara imejenga bweni la wasichana katika shule ya sekondari magara ili kuhakikisha watoto wa kike wanasoma muda wote.