Mkazi wa Kijiji cha Lundusi, Kata ya Peramiho, wilayani Songea, Mkoa wa Ruvuma, Bibi Scholastica Mhagama amejiandalia jeneza lake ambalo litatumika kumzikia siku atakayoaga dunia.


Bibi Scholastica Mhagama(76) ambaye amejiandalia jeneza lake litakalotumika kumzikia.Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita, Scholastica alisema alilitengeneza jeneza hilo zaidi ya miaka mitano iliyopita baada ya kuona anaishi kwa dhiki na anatengwa na baadhi ya watu.
“Nilijitengenezea jeneza langu na fundi alipomaliza kazi, niliingia ndani kupima kama ninatosha, nikajilaza na kuona liko sawasawa,” alisema bibi huyo.


Bibi Scholastica Mhagama akiliangalia jeneza lake.Akifafanua zaidi bi mkubwa huyo alisema ameishi maisha ya dhiki na kunyanyaswa bila msaada kutoka kwa jamii anayoishi, hali ambayo imemfanya amuombe Mungu amchukue ili azikwe kwenye jeneza alilojiandalia.
“Kila siku naomba Mwenyezi Mungu anichukue haraka ili nikapumzike kutokana na mateso ninayoyapata, lakini hofu yangu ilikuwa je nikifa, nitazikwa kama binadamu wengine? Ndiyo maana nimeamua kujiandalia jeneza langu,” alisema bibi huyo mwenye ulemavu wa mguu uliotokana na kung’atwa na nyoka kisha kukatwa huku mwingine ukimsumbua kukunjuka.


Bibi Scholastica Mhagama akiwa ndani ya nyumba anayoishi.Alipoulizwa sababu ya kutengwa na jamii, bibi huyo alisema: “Nimetengwa na jamii na majirani wanashindwa kunisaidia wanadai eti mimi ni mchawi kwa sababu watoto wangu wote wanne walikufa wakiwa wadogo. Naumia sana kusingiziwa kitu ambacho sikijui.’’
Bibi huyo anayeishi katika kibanda kilichoezekwa kwa nyasi anasema kuwa, aliweza kutengeneza jeneza hilo baada ya kupewa shilingi 40,000 na mfadhili mmoja.
“Tayari nilikuwa na mbao, hivyo kazi ilikuwa kumlipa fundi fedha na kumpa mbao ili anitengenezee jeneza,” alisema Scholastica. Bibi Scholastica akiwa nje ya nyumba yake siku alipoongea na mwandishi wetu.
 
Top