KLABU ya Manchester City imemfanya Eliaquim Mangala kuwa beki ghali zaidi kwa sasa katika historia ya soka ya Uingereza, baada ya kumnunua kwa Pauni Milioni 31.9 beki huyo wa kati wa Ufaransa kutoka FC Porto. Ndoto za Mangala kuhamia Ligi Kuu ya England hatimaye zilitimia jana baada ya kuupiku uhamisho wa Pauni Milioni 30 uliomtoa Rio Ferdinand Leeds kuhamia Manchester United mwaka 2002. Mangala,
mwenye umri wa miaka 23, anakuwa mchezaji wa sita kusajiliwa na City baada ya kukubali Mkataba wa miaka mitano na kocha Manuel Pellegrini anaamini huyo ni moja ya mabeki wa thamani ya juu Ulaya na atadhihirisha thamani yake uwanjani.
Beki ghali: Eliaquim Mangala amesaini Manchester City kutoka Porto kwa Pauni Milioni 32. Mfaransa huyo baada ya kukamilisha uhamisho wake amesema; "Mimi ni aina ya mchezaji ambaye naingia uwanjani kushinda,". "Siachi kitu chochote, wakati wote napambana hadi mwisho na nina matumaini kwa desturi yangu huu, tutashinda mataji mengi msimu huu. "Nina furaha sasa kwa sababu nitakuwa tayari kuanza maisha mapya. Nitakuwa tayari kufanya mazoezi tena. Ilikuwa vizuri kwenda mapumziko, lakini baada ya muda unarudi kazini. "Ninakwenda kukimbia kila siku na kufanya mazoezi kwenye gym. Mapumziko ni mazuri, lakini yakiwa marefu, inakuwia vigumu kurudi vizuri. Nafikiri nitahitaji muda, ila nitapambana kurudi katika ubora wangu kwa asilimia 100 haraka iwezekanavyo. "City ni klabu kubwa Ulaya. Kwangu, ilikuwa hatua muhimu kuondoka Porto na kujiunga na Manchester City ili kusonga mbele kimafanikio. Nataka kushinda mataji na ninaamini nitafanya hivyo,"amesema.
 
Top