WAKATI Rais Jakaya Kikwete, akikutana na vyama vya siasa kutafuta maridhiano ya mchakato wa Katiba, Jukwaa la Wakristo Tanzania, limetoa tamko zito lenye masuala sita, likimwomba Rais aliahirishe Bunge Maalum ili kuepusha ishara za aina mbalimbali za kuanzisha sintofahamu nchini na hali yoyote inayoweza kuathiri vibaya mshikamano, umoja na amani ya Taifa.Tamko hilo lilitolewa Agosti 28 mwaka huu, na jukwaa hilo linaloundwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Baraza la Kikiristo Tanzania (CCT) na Jumuiya ya The Seventh Day Adventists (SDA).

“Ifahamike kuwa wananchi wa Tanzania wako juu ya wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi. Kwa mantiki hiyo, tunakuomba uepushe Watanzania kuhamasishwa kukikataa CCM kwa kuwa tu kimeyapuuza na kimekataa maoni yao waliyotoa kwa dhati baada ya kuaswa na kuhimizwa kufanya hivyo na viongozi wa nchi,” linasomeka tamko hilo.

Kwamba, wajumbe wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, tulikutana Agosto 27 hadi 28 Agosti mwaka huu, jijini Dar es salaam na kupata fursa ya kutafakari, kujadili na kujielimisha kwa kina yaliyomo katika rasimu ya pili ya Katiba na mjadala unaoendelea katika Bunge Maalum la Katiba.

“Baada ya mjadala wa kina, tunatoa tamko letu kwa kuipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikusanya maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko hayo na kutuletea rasimu yenye maoni mengi ya Watanzania bila kujali dini zao, upande wa Muungano walikotoka, hali zao za kimaisha, jinsi na kabila.

“Pia tunaipongeza Tume kwa kuandaa nyaraka na kumbukumbu mbalimbali kama Randama, nyaraka zenye maoni ya wananchi, picha, tafiti mbalimbali na hata orodha ya watu walioshiriki kutoa maoni katika Tume,” walisema.

Tamko hilo liliongeza kwua Tume pia iliweza kuandaa Tovuti iliyokuwa na kumbukumbu zake na maoni yote yaliyotolewa, kwamba hii ni ushahidi kuwa tume iliandaa rasimu kwa weledi na kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuzingatia maoni ya wananchi.

“Baada ya Tume kuwasilisha rasimu kwenye Bunge Maalum la Katiba, Taifa likaanza kushuhudia “uasi wote na uovu wa wanadamu wapingao kweli kwa uovu” (Warumi 1:18).

“Katika mijadala ya Bunge Maalum la Katiba yakaanza kujitokeza mambo mengi yasiyo ya maslahi kwa wananchi na ukiukwaji wa sheria na kanuni,” wanasema na kuyataja mambo yanadhihirisha madai yao.

Wanaelez kuwa Tovuti ya Tume ilifungwa bila sababu za msingi kutolewa wakati mchakato unaendelea, hali ambayo imefanya zile nyaraka na kumbukumbu zilizoandaliwa kwa ajili ya rejea na kuwezesha mjadala wa rasimu ya Katiba kuendelea katika mwanga na ufahamu wa nyaraka hizo kutowezekana kabisa.

Kwamba, tumeona Bunge Maalumu la Katiba likiendelea kupotosha takwimu na taarifa mbalimbali ambazo wananchi hawawezi kuzipata kwa ajili ya kuoanisha baina ya kinachojadiliwa bungeni na kilichomo katika rasimu na viambatanisho vyake vyote.

“Tunajiuliza jambo hili limefanywa na nani na kwa maslahi ya nani? Bunge la Katiba limeshindwa kusimamia Kanuni kama ambavyo zilipendekezwa na kuridhiwa na wajumbe wake. Kushindwa huku kusimamia kanuni kumesababisha vurugu ndani ya Bunge na kumekwamisha matarajio ya wananchi kupata Katiba bora ya nchi yetu.

“Matumizi ya ubabe na wingi wa wabunge wa CCM, badala ya Kanuni za Bunge na maridhiano, kumefanya mchakato wa Katiba kuhodhiwa na CCM dhidi ya maslahi ya wamanchi,”walisisitiza.

Jukwaa hilo lilisema kuwa mijadala katika Bunge imekuwa ya kejeli, matusi, vitisho, ubabe na kupuuza hata kupotosha maoni yaliyotolewa na wananchi kwa Tume, jambo lilowafanya baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo kuamua kususia vikao na wengine kuendelea bila kukumbuka kuwa katiba ni matukio ya tendo la maridhiano.

“Hatua iliyofikiwa ni dhahiri, mjadala wa Bunge unaoendelea umeondoa kwa kiasi kikubwa maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu muundo wa Muungano, kupunguza mamlaka ya Rais, uwajibikaji na uwajibishwaji wa wabunge, ukomo wa ubunge na kuwezesha maoni na maslahi ya CCM kwa uongozi wa kikundi cha wanasiasa wachache wasio na uaminifu na uadilifu wa kutosha kuwekwa kama mapendekezo ya Katiba mpya kwa nia ya kulinda maslahi binafsi au ya makundi,” walisema.

Baada ya kujadili na kuona haya, Jukwaa la Wakristo Tanzania limetoa maoni yake na kutaja mambo sita ya kuzingatia ambapo linaitaka serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, irudishe tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na nyaraka zake zote kwa ajili ya wananchi kuendelea kuona kazi waliyoifanya, kujifunza na kujadili rasimu kwa uwazi.

Kwamba, maoni ya wananchi hayawezi kufutwa na kudharauliwa na CCM, hivyo basi, Bunge Maalumu linaloendelea lijadili na kuboresha tu maoni yaliyomo katika rasimu ya Katiba na sio kufanya mabadiliko katika Katiba ya mwaka 1977.

Jukwaa pia linapendekeza mchakato wa Katiba usimamishwe ili kupisha majadiliano, maelewano na maridhiano muafaka, uchaguzi mkuu na wa serikali za mitaa.

“Mabadiliko ya Katiba ya 15 ya mwaka 1977, yafanyike kuwezesha chaguzi kufanyika kwa uwazi na haki. Pia, kuweka kifungu kitakacholinda rasimu ya pili na kumtaka kiongozi ajaye kuendelea na mchakato wa Katiba,” walisema.

Katika sharti la nne, wanasema baada ya Bunge Maalum kuanza shughuli zake tena, Mwenyekiti wake, afanye kazi kwa mujibu wa kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba badala ya kutumia ubabe na kiburi cha wingi wa wajumbe wa CCM.

Pia wananchi wanashauriwa kuendelee kusoma na kujadili maoni yaliyoko katika rasimu ya pili ya Katiba, na kufuatilia kitakachokuwa kinajadiliwa kwenye Bunge la Katiba ili kuwawezesha kupiga kura ya maoni wakiwa na uelewa wa kutosha.

“Tume ya Mabadiliko ya Katiba ihuishwe na kupewa mamlaka kisheria ili kuiwezesha kujibu maswali yanayojitokeza na kutoa ufafanuzi kwa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi kwa jumla hadi Katiba mpya itakapokamilika na kukabidhiwa rasmi,” walisema.

Mkutano na vyama

Taarifa kutoka mkoani Dodoma, zinasema kuwa Rais Kikwete leo atakutana na viongozi wa vyama vya siasa kwa ajili ya kujadili na kutafakari maendeleo ya mchakato wa Katiba mpya chini ya utaribu wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo, aliwaeleza waandishi wa habari katikati ya wiki hii kuwa hatua hiyo ilitokana na kikao chao Agosti 23 makwa huu, ambapo na walikubaliana watafute nafasi ya kukutana na Rais Kikwete.

Habari zilizotulifikia jana jioni, zilisema kuwa Rais atakutana wa viongozi hao kwa siku ya kesho mkoani Dodoma na hivyo mkutano wake na wazee wa mkoa huo umesogezwa mbele hadi Septemab 4 mwaka huu.

TCD inaundwa na vyama vyenye wabunge ambavyo ni CHADEMA, TLP, CUF, NCCR-Mageuzi, CCM, UDP na UPDP inayoviwakilisha vyama visivyo na wabunge.
 
Top