Utaratibu mpya wa Hazina kulipa mishahara moja kwa moja kwa watumishi wa halmashauri, umefichua ‘mchezo mchafu’ wa watumishi waliofariki na watoro kulipwa mishahara.
Akisoma risala ya washiriki mafunzo ya utekelezaji wa awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa washiriki hao, Ramadhani Chomolla, alisema Serikali imepata hasara kupitia utaratibu huo.
Aliitaka Serikali kuangalia upya mfumo wa Hazina wa kuwalipa moja kwa moja watumishi, ili kuepusha hasara hiyo ya kulipa mshahara watumishi waliofariki, watoro na walioacha kazi.
“Mshahara wa Julai (mwaka huu), Hazina imewalipa moja kwa moja watumishi, hivyo watoro na waliofariki nao wamepata mishahara, hii imeiingizia Serikali hasara na watoro wameanza kudharau wakuu wa vituo,” alisema Chomolla.
Hata hivyo, akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema hilo si kosa la Hazina, ila ni halmashauri zenyewe kwa kuwa zinawajibika kupeleka mahitaji ya mishahara na akaunti za watumishi.
“Kama mtumishi amefariki ndani ya mwezi ambao mshahara umelipwa sio tatizo, lakini kama amefariki siku nyingi na amelipwa, hii inaonesha kuwa fedha hizi zingefika kwenye halmashauri zingeliwa na wachache.
“Naamini watu wa aina hii watakuwa wawili au watatu, ikiwa zaidi ya hapo basi halmashauri itakuwa na matatizo. Nadhani safari hii marehemu au walioacha kazi wamewazidi ujanja,” alisema.
Alisema hatua ya Serikali ya kulipa mishahara moja kwa moja, ilitokana na kuwapo kwa mabadiliko ya nyongeza za mishahara na kutaka watumishi walipwe mapema.
“Ni nafuu ya nusu lawama kuliko malalamiko ambayo Serikali ingeyapata kama watumishi wasingelipwa mishahara, kulikuwa na mabadiliko ya mishahara na pia ilikuwa inakaribia Sikukuu ya Idd,” alisema.
Akizungumzia mafunzo hayo, Ghasia aliwataka washiriki kuhakikisha changamoto zilizojitokeza kwenye awamu ya kwanza, hazijirudii katika utekelezaji wa awamu ya pili.
Alisema awamu ya kwanza ilikuwa na changamoto kadhaa, ikiwemo udhaifu katika usimamizi wa fedha, matumizi mabaya ya fedha za miradi na kuchelewa fedha za ruzuku za uendelezaji shule.
“Tumewapa mafunzo kwa pamoja watendaji mnaohusika katika utekelezaji wa mpango huu, hivyo hatutegemei changamoto za awamu ya kwanza kujirudia au kutokuwa na ufanisi katika kutekeleza miradi,” alisema.
Aidha, Ghasia alikemea tabia ya watendaji katika baadhi ya halmashauri kusingizia mfumo wa matumizi ya fedha kwa njia ya mtandao (EPICA), kuwa ndio chanzo cha kukwamisha utekelezaji wa miradi.
Ghasia alitolea mfano wa kushindwa kutumika kwa Sh milioni 897 za mwaka 2012/13 kwa ajili ya uendeshaji wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Kasulu, kwa kisingizio cha mfumo wa Epica, huku fedha hizo zikitumiwa katika matumizi mengine.
“ Linapofika suala la utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Epica inakwamisha, lakini fedha za mishahara, safari au posho Epica inafanya kazi, hali hii hatutaivumilia,” alisema.
Washiriki 411 kutoka halmashauri na mikoa 16 walishiriki mafunzo yaliyotolewa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM). Mikoa hiyo ni Ruvuma, Simiyu, Singida, Mtwara, Lindi, Tanga, Shinyanga, Geita, Morogoro, Arusha, Manyara, Iringa, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Dodoma na Pwani.
Waliopata mafunzo hayo ni maofisa elimu na ofisa mipango wa mkoa na wilaya, wahandisi na waweka hazina wa halmashauri.