Mjumbe wa Bunge la Katiba, James Mapalala ametoa siri ya kutokujihusisha na suala la upigaji kura katika kamati yake namba moja kwa kusema inapigia upatu serikali mbili.Mapalala ambaye ni miongoni mwa waanzilishi wa mfumo wa siasa wa vyama vingi nchini, alisema serikali mbili zimekuwa zikimchefua, hivyo hawezi kushiriki usaliti huo. Katika kamati hiyo, pia yupo Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy aliyejipambanua kuwa haungi mkono mfumo huo unaopigiwa upatu na chama chake.

“Mimi sikutoka bungeni kwa sababu niliamua kupambana mle ndani... kusema kweli nimepambana nikiwa peke yangu na mmoja wa wabunge wa CCM, lakini kila inapofikia hatua ya kupiga kura katika vifungu vya Serikali mbili, mimi najitoa,” alisema Mapalala.

Kwa upande mwingine, mbunge huyo alikitaka Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake kumuomba radhi Jaji Joseph Warioba kwa kumdhalilisha kuhusu masuala ya Rasimu ya Katiba.

Alisema Warioba anatakiwa kuombwa radhi kwa sababu mambo mengi ambayo aliyapeleka katika Rasimu yalitoka kwa wananchi, lakini yameachwa, jambo linaloonyesha kazi yake imekuwa ni ya bure.

Mapalala aliwaponda wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwamba wanafanya kazi ya kutengeneza mfumo wa kugawana posho kwa watu wa Tanzania Bara na Zanzibar.

“Hapa wanafanya mipango na ‘madili’ ya kugawana posho, hatuna jambo jipya humo, tunachotaka sisi tulio wengi ni serikali tatu na wanachokitaka wenzetu wachache ni serikali mbili na migao ya madaraka na fedha, vitu ambavyo vimeshindwa kutuvusha kwa kipindi cha miaka 50,” alisema Mapalala.

Kwa upande mwingine, mkongwe huyo alikituhumu chama hicho kwamba kinafanya mambo kwa kujiaminisha kuwa inaweza kutawala milele.

Hata hivyo, Mapalala amewataka vijana kuwa wajasiri ili utakapofika wakati, waipinge katiba yenye mfumo wa serikali mbili na waunge mkono serikali tatu.

 
Top