Agizo lililotolewa na Rais Jakaya Kikwete, linalotaka ujenzi wa maabara kwenye shule zote nchini ukamilishwe ifikapo Novemba 2014, limeibua hekaheka wilayani hapa.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa, alionya wakuu wa idara za elimu, madiwani na watendaji wa kata watakaokwamisha kwa namna yoyote hatua za kufanikisha agizo hilo, watafukuzwa.Mkwasa alitoa onyo hilo akizungumza na madiwani, watendaji hao kwenye kikao cha Baraza la Madiwani lililoanza kukutana juzi.

“Wasimamizi wakuu wa ujenzi wa maabara hizi ni wakuu wa idara za elimu, madiwani na maafisa watendaji wa kata kwahiyo sitawaelewa ikiwa kutatokea uzembe wa aina yoyote,” alisema.

Alisema ufuatiliaji wake umeonyesha kuzorota kwa utekelezaji wa jukumu hilo, katika baadhi ya kata na kuonya kuwa wakati umewadia ambapo wanaosababisha hali hiyo hawataonewa aibu.

Aliongeza kuwa wakuu wa wilaya na mikoa nchini kote wameagizwa na Rais Kikwete wahakikishe ujenzi huo unakamilika na kuanza kutumiwa na wanafunzi ifikapo Novemba, mwaka huu.

‘‘Kabla sijawajibishwa, mtakuwa wa kwanza kuachia ngazi kwasababu mmepewa muda mrefu kukamilisha ujenzi huo, ikifika Novemba hamjakamilisha, jiondoeni madarakani badala ya kusubiri kuondolewa,”alisema.

Madiwani Jamal Shabiby, wa Kata ya Mtita na Ramadhani Mtawa, wa kata ya Bahi kwa nyakati tofauti wakichangia hoja hiyo kwenye mkutano huo, walisema utekelezaji wa agizo hilo katika baadhi ya kata hautafanikiwa kwakuwa maafisa watendaji wake siyo waaminifu.

“Watendaji katika baadhi ya Kata siyo waaminifu katika matumizi ya fedha zilizochangwa na wananchi kwa ajili ya ujenzi wa maabara,” alieleza Shabiby

Mtawa naye alimueleza Mkwasa kuwa baadhi ya watendaji katika kata wanatumia fedha za ujenzi huo kama vile ni za kwao binafsi na kwamba ndiyo changamoto inatakayokwamisha ogizo hilo la Rais.
 
Top