WAFUNGWA MIAKA 5 KWA KUIBA MLINGOTI WA BENDERA YA TAIFA
Mahakama ya Mwanzo Mengwe imewahuku watu watatu kutumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa mlingoti wenye bendera ya taifa katika kituo cha Polisi Ngoyoni kilichopo Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.
Hukumu hiyo ilitolewa wiki iliyopita na Hakimu wa Mahakama hiyo, Adinan Kingazi baada ya ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kuwatia hatiani washtakiwa hao.Waliohukumiwa kwa kuiba mlingoti huo wa chuma wenye thamani ya Sh. 80,000 mali ya jeshi hilo ni Alphonce Assenga, August Moris na John Ngowi, wakazi wa kijiji cha Ngoyoni kata ya Mengwe wilayani humo.
Hakimu huyo alifafanua kuwa mshtakiwa wa kwanza Alphonce atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela na wa Pili na watatu miaka miwili ili iwe fundisho kwa watu wengine.