RAIS OBAMA na VIONGOZI AFRICA:- Nchi 6 kuimarisha usalama wa Afrika ni pamoja na Ghana, Rwanda, Senegal, Tanzania, Ethiopia na Uganda.
Sehemu ya wajumbe wa Mkutano wa Viongozi wa Nchi 50 kutoka Afrika na Marekani ambao umewakutanisha na Rais Barak Obama katika ukumbi wa State Department jijini Washington DC Agost 6, 2014…
Viongozi hao wa Afrika walikuwa na mazungumzo mjini Washington jumatano Agost 06,2014, kuhusu kupanua biashara, kuimarisha usalama na kuboresha uwajibikaji wa serikali kote barani Afrika.
Mazungumzo hayo ni katika mifululizo ya mikutano iliyofanyika ikiwa ni kilele cha mkutano mkubwa wa siku tatu unaowashirikisha wakuu wa mataifa 50 kutoka barani Afrika. Katika matamshi yake ya ufunguzi hapo jumatano, Rais Obama alisema Afrika mpya inajitokeza. “Huku baadhi ya chumi zikikua haraka sana duniani, ukuaji wa daraja la kati na vijana na ukuaji wa haraka sana wa idadi ya watu duniani, Afrika itasaidia kujenga muundo wa dunia ambao haujawahi kuwepo awali”.
Rais alisema kuongezeka fursa za biashara barani Afrika kutasaidia kuandaa uhusiano kati ya Marekani na bara la Afrika.
Rais Obama ametangaza dola bilioni 33 katika uwekezaji binafsi na wa umma nchini Marekani kwa mataifa mbali mbali barani Afrika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry anaelekeza namna ya
kutumia kipaza sauti baada ya Rais Obama kufungua mkutano huo, wakati
mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Rais Mohamed Ould Abdel Aziz alipoongea kwa niaba ya Viongozi wa Afrika.
Rais wa Tanzania ,Dr.Jakaya Kikwete na viongozi wenzake wa Afrika katika mkutano wa Viongozi wa Afrika na Marekani ambao uliwakutanisha na Rais Barak Obama katika ukumbi wa State Department jijini Washington DC Agost 6, 2014. Miongoni mwa waliohudhuria pia ni Rais Paul Kagame wa Rwanda, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Goodluck Jonathan wa Nigeria, Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini.
Rais Barack Obama wa Marekani, amesema nchi yake itayasaidia mataifa ya Afrika kuunda kikosi cha dharura kitakachovisaidia vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
Akihitimisha mkutano kati yake na viongozi wa nchi 50 wa Afrika mjini Washington, Rais Obama amesema kikosi hicho kinaweza kupelekwa haraka kuvisaidia vikosi vinavyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa barani Afrika.
Amesema nchi sita zitakazohusishwa katika kuimarisha usalama wa Afrika ni pamoja na Ghana, Rwanda, Senegal, Tanzania, Ethiopia na Uganda.
Taarifa ya Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa nchi hiyo itatumia Dola milioni 110 kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitatu hadi mitano, kusaidia kuundwa kwa kikosi kipya.
Hata hivyo, Rais Obama hakufafanua ni vipi kikosi hiko cha kulinda amani kitakavyohusiana na vikosi vya sasa vya Umoja wa Afrika.
Hapo jana, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Kerry aliwaonya viongozi hao kwamba makundi ya siasa kali ni kitisho kikubwa kwa uchumi unaokuwa barani Afrika, kwani yanawalenga vijana wengi wasiokuwa na ajira.
Kerry alisema kwamba idadi ya watu milioni 700 wenye umri wa chini ya miaka 30 walioko Afrika, haijawahi kukutikana popote pale kwenye historia ya ulimwengu, na hivyo ni wajibu wa viongozi wa Afrika kulilinda kundi hilo lisiangukie mikononi mwa makundi kama vile Boko Haram la Nigeria na al-Shabaab la Somalia.
Habari Na:-DW Swahili.