Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Fulgence Ngonyani na dereva wake, Nuaka Seme wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Njombe ya Kibena baada ya kupata ajali ya gari iliyomuua mlinzi wa kamanda huyo, usiku wa kuamkia jana, eneo la kiwanda cha miwati (TANWAT).

Ngonyani akizungumza hospitalini hapo, alisema ilitokea kati ya saa tatu na saa nne usiku katika barabara ya Makambako -Njombe.

Alimtaja mlinzi wake aliyekufa ajalini kuwa ni Konstebo George Stephano Matiko (24).

Naye dereva Nuaka, alisema akiwa anaendesha gari la Polisi lenye namba za usajili PT 2058 alivaana na lori ambalo dereva wake aliendesha akiwa katikati ya barabara na baada ya kumwashia taa zote, alijaribu kuhamia upande wake lakini hakufanikiwa kunusuru ajali baada ya kukwanguana.

“Mara baada ya kukwanguliwa tulilikwepa lori tukaigonga nguzo ya umeme na hapo hapo mwenzetu akafa na tunashukuru sana wafanyakazi wa kampuni ya Tanwat ambao waliwahi kuja kutusaidia... na lile lori hatukuweza kuchukua namba zake na liliendelea na safari.”
 
Top