Mwanamme asiyejulikana jina wala makazi yake anayekadiriwa kuwa na umri kati ya 28 hadi 30 (PICHANI) amenusurika kufa baada kupigwa fimbo,virungu na mawe na wananchi kutokana na kile kilichodaiwa kuwa alikutwa akifanya jaribio la kubaka mtoto wa mwenye umri wa miaka mitano nje ya nyumba karibu na choo.

Tukio hilo limetokea jana majira ya saa 11 jioni katika mtaa wa Mwamala kata ya Masekelo katika manispaa ya Shinyanga ambapo mwanamme huyo ambaye hakujulikana jina wala makazi yake alikamatwa na wananchi kisha kuanza kupigwa baada ya kutuhumiwa kutaka kubaka mtoto(jina tunalihifadhi).

Walioshuhudia tukio hilo walisema mwanamme huyo ambaye siyo mwenyeji wa mtaa huo alikutwa akimchezea sehemu za siri mtoto huyo kisha kuanza kumvutia eneo la chooni.

“Alimwita mtoto huyo,akaanza kumchezea sehemu za siri lakini mtoto alipiga kelele na baada ya kusikia kelele za mtoto huyo tukatoka nje kumsaidi, tukapiga mayowe kuomba msaada,watu wakajaa wakaja pia viongozi wakiwemo wa sungusungu wakaanza kumhoji”,alieleza mmoja wa mashuhuda hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

“Hata hivyo mtuhumiwa huyo katika hali ya kubabaika alianza kukimbia na alipoulizwa anatoka wapi hakueleweka mara aseme anatoka Majengo,mara Nguzo nane,mara Buhangija ndipo wananchi wakaanza kumpiga”,alieleza shuhuda huyo.

Akizungumzia tukio hilo bibi wa mtoto aliyenusurika kubakwa bi Marieta Mkaima ambaye hakuwepo wakati tukio hilo alieleza kusikitishwa na kitendo hicho huku akiitaka jamii kuendelea kushirikiana katika kulinda watoto dhidi ya watu wabaya.

“Naishi na mjukuu wangu,sikuwepo nyumbani nimepigiwa simu kuwa kuna tukio nyumbani,ndiyo nimekuta umati wa watu,mwanamme alitaka kubaka mjukuu wangu”,alieleza bibi wa mtoto huyo.

Kamanda wa sungusungu mtaa wa Mwamala Anthony Shija aliiambia malunde1 blog alipigiwa simu na kuambiwa kuwa mwanamme huyo alikuwa amebeba mtoto na kuanza kumshika shika sehemu za siri lakini mtoto katika kujihami kwake mtoto alifanikiwa kumponyoka mikononi mwa mtuhumiwa huku akipiga kelele.
“Baada ya mtoto kuondoka mikononi mwa mtuhumiwa jamaa alimvuta tena ili akidhi haja zake,mtoto akaendelea kupiga kelele ndipo majirani wakajitokeza kumsaidia na kutokana na wananchi kuchoshwa na matukio ya ukatili dhidi ya watoto ndiyo maana wakajitokeza kwa wingi”,alieleza kamanda wa sungusungu.

“Tumepiga simu polisi,tumekuta anapigwa na wananchi,sisi viongozi tumejitahidi kuzuia mtuhumiwa asiuawe kwani wananchi wana hasira sana,wengine wamebeba mawe,fimbo na virungu”,alifafanua kamanda wa sungusungu.

Naye diwani wa viti maalum kutoka kata ya Masekelo bi Zainabu Kheri alilaani kitendo kilichofanywa na mwanamme huyo huku akiitaka jamii kuimarisha ulinzi kwa watoto bila kujali ni wako au la kwani vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hivi sasa ni tishio katika manispaa ya Shinyanga.

“Nikiwa kama mzazi nawaomba wazazi wenzangu na jamii kwa ujumla kulinda watoto,pia wanaofanya vitendo hivi waache tabia hizo na wamwogope mungu pia,kwani ni laana kubwa kubaka,kulawiti na kutoboa macho watoto wasiokuwa na hatia”,alieleza diwani huyo.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa wanamshikilia mtuhumiwa na uchunguzi unaendelea.

“Tulipata taarifa kuhusu wananchi kujichukulia sheria mkononi,tukaenda kumwokoa mtuhumiwa,sasa tunamshikilia,na uchunguzi zaidi unaendelea”,alieleza kamanda Kamugisha.

Tukio la mtoto kunusurika kubakwa limekuja ikiwa ni siku chache tu baada ya mtoto Hapiness Kashinje aliyekuwa anasoma darasa la tatu katika shule ya Msingi Negezi iliyopo kata ya Mwawaza manispaa ya Shinyanga kuuawa kwa kubakwa kisha kutobolewa macho Agosti 25 mwaka huu katika kitongoji cha Kashampa kijiji cha Nhelegani kata ya Kizumbi manispaa ya Shinyanga.

Na Kadama Malunde-Shinyanga
 
Top