Mahakama ya wilaya Nkasi mkoani Rukwa imemhukumu Moses Kang’ombe (17) mkazi wa kijiji cha Karundi wilayani Nkasi kuchapwa viboko 20 kutokana na makosa mawili yaliyokuwa yakimkabili ya kubaka na kumsababishia ujauzito mwanafunzi wa darasa la saba Scolastika Mwanalinze (16) katika shule ya msingi Karundi na kupelekea kutofanya mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka huu.
Akitoa hukumu hiyo mbele ya mahakama hiyo hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya Nkasi Ramadhani Rugemalila alisema mahakama imemkuta na hatia mtuhumiwa baada ya yeye kukiri kutenda kosa hilo na kumtia hatiani chini ya kifungu cha 130 (1) na (2)( e) na 131 (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Alisema katika kosa la kwanza la kubaka atachapwa viboko 12 na kosa la pili la kumpa ujauzito mwanafunzi huyo atachapwa viboko 8 na kesi hiyo haikuhitaji mashahidi baada ya mkosaji mwenyewe kukiri kutenda kosa hilo.

Awali mwendesha mashitaka wa jeshi la polisi Hamimu Gwelo aliiambia mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo mwaka huu na baada ya mwanafunzi huyo kukutwa na ujauzito ndipo alipokamatwa na kufikishwa katika mahakama hiyo na kuwa amevunja sheria chini ya kifungu cha 130 (1) na (2) (e) na 131 (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Aliiomba mahakama hiyo iweze kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa huyo hasa baada ya vitendo hivyo vya ubakaji na kuwasababishia ujauzito wanafunzi ili liwe ni fundisho na kwa wengine wenye nia ya kufanya vitendo hivyo haramu

Mahakama hiyo imetoa hukumu hiyo kwa kuzingatia kuwa mtuhumiwa huyo alikua chini ya umri wa miaka 18.

Na Walter Mguluchuma-Sumbawanga
 
Top