Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza kuanza kutoa vyeti mbadala kwa gharama ya Sh100,000 kwa wote ambao vyeti vyao vimeharibika kiasi cha kutofaa kwa matumizi.
Tangazo hilo lililotolewa jana Septemba 29,2014, na Necta, linawalenga wote waliohitimu elimu zao kuanzia Oktoba 2008, ambao vyeti vyao vina picha za watahiniwa husika, huku likifafanua kuwa waliomaliza kabla ya hapo, utaratibu wa kuwatumia uthibitisho wa matokeo katika taasisi zenye mahitaji utaendelea.
Kwa mujibu wa tangazo hilo: “Ombi la cheti mbadala litapokewa baada ya miezi mitatu kupita tangu upotevu wa cheti halisi kutangazwa gazetini.

Uchunguzi wa uthibitisho utafanyika kwa siku 30 tangu kupokewa kwa ombi la cheti mbadala kwa kuihusisha polisi (kitengo cha uchunguzi wa picha).”

Katika kukabiliana na udanganyifu unaoweza kujitokeza kutoka kwa watu wasio waaminifu, baraza hilo lilisema kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaoshiriki katika uombaji wa vyeti hivyo vitakavyokuwa na neno ‘duplicate’ ili kuvitofautisha na vyeti halisi.
“Cheti mbadala kitatolewa mara moja tu na endapo itabainika kuwa cheti halisi bado kinatumika katika soko la ajira au mafunzo na mtahiniwa akathibitika kushiriki katika kuidanganya Necta, hatua kali za kisheria zitachukuliwa,” inaonya fomu ya maombi ya cheti.

Waliopoteza vyeti halisi watatakiwa kutoa taarifa polisi na kutangaza gazetini, huku waliounguliwa au vyeti vyao kuharibiwa na mchwa, mafuriko, panya au kwa namna nyingine yoyote watatakiwa kuwasilisha vielelezo husika pamoja na barua ya Serikali ya Mtaa wa eneo la tukio la moto au mafuriko yalipotokea.

Taarifa hiyo ilisema kuwa, iwapo yapo mabaki ya cheti husika, watatakiwa kuyawasilisha Necta.

Tangazo la gazetini la upotevu wa cheti litatakiwa kuwa na taarifa muhimu kama jina la mtahiniwa, namba ya mtihani, aina ya mtihani, mwaka wa mtihani, jina la shule na picha ya mtahiniwa.

Baada ya polisi kutoa hati ya upotevu wa cheti, mwombaji atatakiwa kuambatanisha picha ndogo mbili pamoja na nakala ya kitambulisho na risiti halisi ya malipo.

Pia, katika mwendelezo wa kujiridhisha kuwa kila mtumishi au mwanafunzi anakuwa na cheti chake baada ya taasisi mbalimbali pamoja na idara za Serikali kuanzisha utaratibu wa kuhakiki taarifa za kitaaluma hasa vyeti vinavyotolewa na baraza hilo.
 
Top