Mahakama ya Ardhi na Nyumba Wilaya ya Arusha, imeamuru maiti iliyozikwa Septemba 15, mwaka huu kwenye eneo lenye mgogoro lililoko katika kijiji cha Ngaramtoni, wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, ifukuliwe. 
Mahakama hiyo imeamuru mwili huo ufukuliwe kutoka katika shamba hilo ambalo ni la marehemu Francis Kivuyo na ukazikwe eneo jingine lisilo na mgogoro wa ardhi. Hukumu hiyo iliolewa mwishoni mwa wiki na Hakimu wa Mahakama ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ya Arumeru, Doris Mangure, kufuatia kesi iliyofunguliwa na mtoto wa mmiliki wa shamba hilo, Thomas Kivuyo (32). 
Thomas aliiomba mahakama hiyo kutoa uamuzi wa maiti kufukuliwa kutoka katika shamba hilo ili aliendeleze. 
Katika kesi hiyo, mlalamikaji aliwakilishwa na kampuni ya uwakili ya Mwaluko Advocate Company ya jijini hapa. 
Ilidaiwa kuwa mwaka 1987, marehemu Kivuyo alikodisha shamba hilo kutoka kwa Kurosoi Loilole (70) na mwaka 1989 kupitia uongozi wa kijiji cha Ngaramtoni, alinunua shamba hilo lenye ukubwa wa ekari mbili. 
Mwaluko aliiambia mahakama hiyo kuwa mwaka 2006, ndipo chokochoko dhidi ya mteja wake na usumbufu vilipoaanza kutoka kwa mlalamikiwa Loilole. 
Alidai kuwa mlalamikiwa huyo alirubuniwa kwa lengo la kuliuza shamba hilo kwa wanunuzi wapya kutokana na ardhi kupanda thamani kijijini hapo, hatua ambayo ilimlazimu mlalamikaji kufungua kesi mahakamani ya kuzuia kubughudhiwa. 
Mwaluko alidai kuwa mwaka 2006, mteja wake marehemu Kivuyo, baada ya kuuziwa shamba hilo alipanda mazao, miti na kuweka uzio wa miti kuzunguka shamba lote na ndipo alipoanza 
kusumbuliwa na aliyemuuzia shamba hilo, hatua iliyosababisha aende mahakamani kufungua kesi. 
Alidai kuwa mtuhumiwa naye alifungua kesi mahakamani akiomba shamba hilo lisitishwe kutumika katika kesi hiyo hata hivyo, alishindwa kukidhi vigezo.
 
Top