CHAMA Cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), Wilaya ya Mtwara Mjini, jana walishindwa kuandamana baada ya Jeshi la Polisi mkoani hapa, kuwashikilia viongozi wa chama hicho kuanzia saa moja asubuhi hadi sita mchana.
Maandamano hayo yalitarajiwa kufanyika kuanzia maeneo ya Makanaledi kupitia Mnarani, barabara ya Zambia, Stendi Kuu, Madukani, Bima, Coco Beach hadi viwanja vya Mashujaa, ambako wangezungumza na wananchi, lakini yalidhibitiwa na polisi ambao walionekana wakirandaranda kila kona pamoja na magari ya JWTZ kuhakikisha hakuna maandamano hayo.
Viongozi walioshikikiwa na polisi ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mtwara Mjini, Ibrahimu Mandoa, Mkufunzi Chadema Mkoa, Ismail Liuyo, Katibu Stanslaus Sumi na Katibu Mwenezi Hassani Mbangile.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kutoka kituo cha Polisi Wilaya, Mwenyekiti huyo wa Wilaya, Ibrahimu Mandoa, alisema jana Chadema Wilaya walikusudia kufanya maandamano ya amani katika Manispaa ya Mtwara-Mikindani kupinga kuendelea kwa Bunge maalum la Katiba linaloendelea Dodoma.
Alisema kuwa, kimsingi kila mtu atakuwa anaelewa kuwa Rais Kikwete na vyama vya siasa ambavyo viko chini ya TCD, walikuwabaliana kwa pamoja kwamba hakuna uwezekano wa kuweza kupatikana Katiba mpya sasa hivi mpaka 2016 ndio zoezi la mchakato mzima liendelee.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Augustine Ollomi, alithibitisha kukamatwa kwa viongozi hao na kuhojiwa kwa sababu ya kusambaza vipeperushi kwa wananchi.
Ollomi, alisema kuwa viongozi wa Chadema walitoa taarifa ya kufanya mkutano Septemba 21, lakini Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Andrew Ndassa, aliwakatalia kwa sababu zilizotolewa zilikuwa kinyume, wao walitaka kufanya mkutano kupinga Bunge maalumu ambalo linaendelea Dodoma, na kwa ufahamu wake bunge hilo liko kisheria sio kama wanavyodai Chadema.
Alisema, juzi walipata vipeperushi ambavyo vilikuwa vimeandaliwa na viongozi Chadema mkoani hapa wakiwashawishi wananchi washiriki katika maandamano, hivyo ndio sababu ya kuwaita kwa ajili ya mahojiano.