MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, amehamishia vita vya maneno Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akidai kuwa viongozi wake wameweka namba yake ya simu kwenye tovuti ili atukanwe na wananchi kila siku. 

Sitta, alitoa tuhuma hizo bungeni mjini hapa jana asubuhi, wakati
akimpa nafasi Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema, ili atoe ufafanuzi wa hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyofunguliwa na mwandishi Saed Kubenea dhidi ya AG akiomba tafsiri ya kifungu cha 25 (1) (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu kazi ya Bunge Maalum. 

“Waheshimiwa wajumbe, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilitoa hukumu kuhusu shauri lililofunguliwa na Kubenea dhidi ya AG…na baada ya hukumu hiyo kutoka kumekuwa na taarifa ambazo nyingine zinashangaza na hasa
kwa baadhi ya wenzetu wa katika tasnia ya habari, wameamua kuendelea kulipiga vita Bunge hili lisiendelee kwa njia yoyote. 

“Sasa kuondoa hali hii, na pengine hata hili watapotosha, namuita AG afafanue hukumu hiyo,” alisema Sitta na kisha Jaji Werema kujongea mbele na kuisoma hukumu hiyo iliyoandikwa kwa Kiiingereza, halafu akaitafsiri kwa Kiswahili. 

Baada ya Jaji Werema kumaliza, Sitta aliinuka tena akasema;
“Nakushukuru AG kwa ufafanuzi huo…wale wanaotaka kusema mengine waendelee kwa sababu ndio uhuru uliopo katika nchi yetu, hatuwezi kuwazuia,”. 

Sitta aliongeza kuwa; “Labda niseme moja, wale wenzangu katika vyombo vya habari ambao wananichukia mimi binafsi, wasichanganye chuki hizo na mchakato wa Bunge Maalum. 

“Mimi ninapokea matusi kila siku, sms zisizopungua 50…viongozi wa CHADEMA wameweka namba yangu ya simu katika tovuti nitukanwe kila siku. Hilo mimi niko tayari na naliona sawa, sihangaiki nalo,” alitamba. 

Sitta alisisitiza kuwa, Bunge hilo ni chombo kilichoanzishwa kikatiba na kwamba kiko tofauti na Mwenyekiti wake. Na kwamba huwezi kuadhibu Bunge Maalum kwa sababu hupendi sura ya Mwenyekiti wake. 

“Mimi wale wanaotaka mapambano, tuendelee kupambana lakini kazi ya Bunge Maalum itaendelea na ndugu zangu Watanzania wajue tunaandaa Katiba bora na lazima itapatikana,” alisema na baada ya muda mfupi wakati kamati zikiendelea kuchambua mapungufu yaliyomo kwenye rasimu inayopendekezwa, alikatiza na kusema; 

“Ujumbe kutoka kwa wenzetu walioyoko hija; Tunawatakia kila la heri katika kutimiza kazi mliyopewa na taifa na tunawahakikishia kuwa tuko tayari kupiga kura wakati wowote. 

Nimeishoma hiyo ili wale wanaopigapiga kelele huko nje wajue kuwa tumepania kweli kweli hatufanyi mzaha hapa Dodoma,”.

via >>TANZANIA DAIMA
 
Top