Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Mh. Freeman Mbowe jana amehojiwa na jeshi la Polisi nchini Tanzania kuhusiana na kauli alizozitoa katika mkutano mkuu wa chama hicho hivi karibuni huku vurugu zikitawala katika tukio hilo.
Akizungumza baada ya Mahojiano hayo Wakili wa Chama hicho Mh. Tundu Lisu amesema mahojiano na mwenyekiti huyo yalienda vizuri na salama kwa ushauri wa jopo la mawakili wanaomuwakilisha kiongozi huyo wa kambi ya Upinzani.

Vurugu zilizuka muda mfupi baada ya Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – Chadema, Freeman Mbowe, kuwasili kwa ajili ya mahojiano ambapo Awali vurugu hizo zilihusisha wafuasi wa Chadema na askari wa kutuliza ghasia FFU, lakini ghafla zikabadilika na kuwa kati ya polisi na waandishi wa habari, hatua iliyotokana na polisi kuanza kuwapiga waandishi na kuwafukuza kwa kutumia mbwa maalumu, kitendo ambacho kimelalamikiwa na waandishi waliokuwepo eneo hilo.

Tukio la kupigwa kwa waandishi wa habari, limetokea siku moja baada ya Makamu wa Rais Dkt Mohammed Gharib Bilal, kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama likiwemo jeshi la polisi, kufanya kazi kwa ushirikiano na wanahabari, kutokana na pande zote mbili kuwa na jukumu moja kuu la kuwatumikia Watanzania.

Katika hatua nyingine huko mkoani Dodoma wafuasi wa nne wa chama hicho wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani humo baada ya kubainika kuwa walikua wanataka kufanya maandamano ambayo kwa mujibu wa jeshi la polisi ni kinyume cha sheria.
 
Top