Tume ya vyuo vikuu nchini Tanzania imesitisha udahili wa wanafunzi wapya katika chuo kikuu cha IMTU kwa mwaka wa masomo 2014/15 na kukipa muda wa miezi 3 chuo hiko kurekebisha kasoro zinazojitokeza mara kwa mara ikiwemo kudahili wanafunzi wengi.
Akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dar es salaam leo Kaimu katibu mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Prof. Magishi Mgasa amezitaja kasoro nyingine zilizopelekea tume hiyo kukifungia udahili chuo hicho ni pamoja na kuendesha program ya ngazi ya cheti bila ya ithbati ya TCU sambamba na kukaidi agizo lilitolewa na Tume hiyo la kusitisha programu hiyo.
Amesema katika kipindi cha miezi mitatu ambacho chuo hicho kitakuwa kimesimamishwa kufanya shughuli za udahili TCU itakuwa ikikifuatilia kwa karibu kuona iwapo chuo hicho kitatekeleza na kufuata taratibu zinazotakiwa.