Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo imetoa hukumu ya kesi ya namba 28 ya mwaka 2014 ambayo iliitaka mahakama hiyo kutoa tafsri sahihi ya mamlaka na mipaka ya Bunge maalum ya katiba iliyofunguliwa na mwandishi wa Habari Saed Kubenea.
Akisoma hati ya amri ya mahakama Jaji Augustino Mwarija kwa niaba ya majaji watatu waliosikiliza shauri hilo,amesema kumekuwepo na Utata katika kifungu cha 25(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 katika lugha mbili zilizotumika kuandika sheria hiyo. Na kusema kuwa kutokana na kifungu hicho kinaipa mamlaka bunge maalumu la Katiba kuijadili rasimu ya katiba,kubadili au kuboresha na kuwa Bunge hilo lina mipaka kwa kuzingatia kifungu cha 9(2) cha sheria ya mabadiliko ya katiba.
Akizungumza baada ya amri hiyo nje ya mahakama kuu Wakili wa Saed Kubenea, Peter Kibatala amesema wanafurahi kuona mahakama imetoa maamuzi kwa wakati na kueleza kuwa tasfiri iliyotolewa ni katika kusaidia wananchi kupata katiba iliyotokana na maoni yao.
Katika kesi hiyo, Kubenea aliiiomba mahakama itoe tafsiri sahihi ya Mamlaka ya Bunge la Katiba kwa kuzingatia kifungu cha 25 (1) na (2) cha Sheria ya Marekebisho ya Katiba Namba 83 ya mwaka 2011. na kuiomba Mahakama itamke kama Bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.