Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa kituo cha redio jamii Uvinza FM chini ya ufadhili wa Shirika la UNESCO na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania.
Wanaoshuhudia tukio hilo kutoka kulia ni Meneja wa huduma za kijamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi, Mwalikishi wa Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambaye pia ni mshauri na mkufunzi wa redio jamii Bi Rose Haji Mwalimu pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Uvinza FM Radio Bi. Nuru Kalufya.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya amesisitiza uadilifu katika vyombo vya habari jamii kwa kutangaza habari zisizoumiza hisia kwa wananchi wengine na kuepuka migogoro.

Akizindua kituo cha redio jamii cha Uvinza FM, Septemba 30,2014,Luteni Kanali Mstaafu Machibya alisema kuwa vyombo vina wakati mgumu hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015.
“Changamoto hii inaweza kuepukika kwa kuhakikisha habari zinazotolewa zinalenga kuendeleza utamaduni wa amani, upendo, utulivu na uvumilivu na kuepuka viashiria vinavyoweza kusambaza chuki kwa lengo la kufanikisha chaguzi salama.

Mkuu wa Mkoa huyo amesisitiza umuhimu wa kuutumia uhuru wa kutoa na kupata habari vizuri kwa kusema kwamba uhuru huo usitumike kutoa habari zinazopendelea upande mmoja na kukandamiza mwingine kwa kuwa hali kama hiyo husababisha machafuko.

“Kwa mujibu wa Ibara ya 18 (b) ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kila mtu anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi, lakini haki hiyo iende sambamba kwa kuzingatia Sheria za nchi na kuhakikisha habari hizo haziumizi hisia za wananchi wengine,”




Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya akisaini kitabi cha wageni ndani ya studio za redio jamii Uvinza FM.


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya akifanyiwa mahojiano mafupi ndani ya studio za redio jamii Uvinza FM na Mtangazaji wa kituo hicho, Kadisilaus Simon mara baada ya kuzindua rasmi redio hiyo.


Mtangazaji wa kituo cha redio jamii Uvinza FM, Kadisilaus Simon akitekeleza majukumu yake kwa furaha kabisa mara baada ya kupewa baraka na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya.


"Hongereni sana UNESCO serikali inatambua mchango wenu",...... Ni maneno ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya akimpongeza Mshauri na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambao ndio wadhamini wakuu wa redio jamii Uvinza FM, Bi. Rose Haji Mwalimu kwa niaba ya UNESCO. Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Uvinza FM Radio Bi. Nuru Kalufya.

Chombo hicho kimetakiwa kutumika kuwaunganisha wanajamii, kuepuka kutangaza hisia au uvumi kwa kueleza ukweli na kuwatunzia heshima wasikilizaji wao kwa kuwa wana haki ya kuheshimiwa na kutoumbuliwa masuala yao binafsi.

Uzinduzi huo umeshuhudiwa pia na Mkuu wa wilaya ya Uvinza Mheshimiwa Mwalimu Hadijah Nyembo, viongozi wa chama na serikali, viongozi wa dini, Shirika la Umoja wa Mataifa (UNESCO), Kampuni ya simu za mkononi AIRTEL, wanakijiji na wananchi wa halmashauri ya Uvinza.

Wengine ni wanahabari 30 wanaohudhuria mafunzo ya maadili, jinsia na habari za migogoro kijijini Uvinza, kutoka redio jamii za wilaya 8 ambazo ni Karagwe, Bunda, Mwanza, Kahama, Sengerema, Maswa, Simanjiro, Loliondo, Mpanda, Ngara. Kutoka Zanzibar ni Unguja North, na Southern Pemba (Pemba).



Mkurugenzi Mtendaji wa Uvinza FM Radio Bi. Nuru Kalufya akitoa neno la shukrani kwa mkuu wa mkoa na wadhamini wa kituo hicho cha redio jamii Uvinza FM.


Meneja wa huduma za kijamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi, akitoa salamu kwa wakazi wa wilaya ya Uvinza kutoka kampuni ya simu za mkononi ya Airtel ambao wametoa udhamini wa mnara wao kurusha matangazo ya kituo cha redio jamii Uvinza FM ili kupanua wigo wa usikivu kwa redio hiyo.


Baadhi ya waandishi wa habari kutoka redio mbalimbali za jamii waliokuwa wakihudhuria warsha ya siku nane iliyokuwa ikiendelea kwenye kituo cha redio jamii Uvinza FM na wakazi wa wilaya hiyo waliohdhuria sherehe za uzinduzi wa kituo hicho.


Baadhi ya viongozi wa dini na jeshi la polisi waliohudhiria uzinduzi huo...Kutoka kulia ni Sheikh Mkuu wa wilaya ya Uvinza Hassan Hamisi, OCD wa Wilaya ya Uvinza S.P Nobert Mahala, Mchungaji wa SDA, Pius Mutani, Mchungaji wa EAG Uvinza, Daniel Magunge na Diwani wa kata ya Ngumka, Abdallah Masanga.
 
Top