MFANYAKAZI wa kiwanda cha kutengeneza vyuma na plastiki cha Lodhia Group of Companies, kilichopo Njiro jijini Arusha, Daniel Godwin(29), amenusurika kupata upofu baada ya kudai kuwa mmoja wa waajiri wake amemwagia maji usoni yanayodaiwa kuwa ni ya betri wakati akidai mshahara wake.
Godwin anadai kutendewa ukatili huo, asubuhi ya Desemba tano mwaka huu, wakati akihoji kwa mwajiri wake huyo sababu za yeye kufutwa kazi kinyemela, sanjari na kutaka kujua hatima ya madai yake ukiwemo mshahara wake wa mwezi uliopita.
Alieleza kuwa tayari ameripoti tukio hilo katika Kituo Kidogo cha Polisi Them na kufunguliwa jalada namba,THM/RB/314/2014.Hata hivyo, alidai kuwa ameshangaa kuona polisi wanashindwa kumkamata mtuhumiwa huyo ambaye ni raia wa kigeni (jina tunalihifadhi).
“Nilianza kufanya kazi katika kampuni hiyo mwaka 2010, katika idara ya matenki nikiwa ni fundi wa kuyatengeneza, hata hivyo, nilishangaa kuona bosi wangu mmoja akianza kunichukia bila sababu.
‘’Sikujali sana kwani niliendelea kufanya kazi hadi hapo siku hiyo nilipofika kazini asubuhi nilikuta jina langu limefutwa kwenye daftari la mahudhurio,’’alidai.
Alisema aliamua kwenda kwa meneja wa kiwanda hicho aliyemtaja kwa jina la Herode Biliamtwe ili kujua sababu za jina lake kuondolewa, alimwambia aende kwa mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Tawi la Kiwandani (TUICO) aliyemtaja kwa jina moja la Hassan, ambapo naye alimtaka arejee kwa bosi wake.
‘’Nilirudi tena kwa bosi wangu na kumweleza lakini cha kushangaa alianza kunitukana kisha kunimwagia maji usoni ambayo baadaye niligundua yalikuwa ya betri, ndipo nilipoenda polisi,‘’ alidai.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Liberatus Sabas alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya tukio hilo alisema hajapata taarifa lakini alisisitiza kuwa jeshi la polisi halina urafiki na mhalifu na aliahidi kulifuatilia sakata hilo.
via>GPL