Marehemu Mwanaisha Mohamed Mbegu ‘Aisha Madinda’enzi za uhai wake.Baada ya danadana nyingi, hatimaye mwili wa mnenguaji Aisha Madinda unafanyiwa upasuaji muda huu katika hospitali ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na mtandao Saluti5, mkurugenzi wa Aset Asha Baraka amebainisha kuwa upasuaji umeanza dakika 10 zilizopita na ni zoezi linalotarajiwa kuchukua masaa mawili.
Asha Baraka amesema baada ya zoezi hilo, watauosha mwili wa marehemu katika msikiti ulioko hapo Muhimbili ikiwa ni pamoja na uvishaji wa sanda kabla ya kuelekea nyumbani kwao Kigamboni.
Mazishi ya Aisha Madinda yatafanyika Kigamboni makaburi ya Kibada leo mchana muda wowote baada ya sala ya Ijumaa kutegemea na namna zoezi la Muhimbili litakavyokamilika mapema.
Upasuaji wa mwili wa Aisha Madinda ulitarajiwa kufanyika tangu saa 1 asubuhi, lakini wakati daktari akiwa ameshafika, polisi aliyetakiwa kusimamia zoezi hilo akachelewa kufika.
Ilibidi Asha Baraka aende hadi kituo cha polisi cha Oysterbay kuonana na polisi aliyetakiwa kusimamia uchunguzi wa Aisha Madinda na ndipo askari huyo akaondoka kuelekea Muhimbili.
Upasuaji huo ulishindikana jana mchana kwa madai ya kuwa muda wa kufanya upasuaji umekwisha na kama si juhudi za Asha Baraka basi hadithi ya jana ingejirudia tena.
(HABARI: SAID MDOE, SALUTI5)