Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Peter Pinda akifafanua jambo.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema serikali imeamua kutafuta soko la utalii kutoka nchi za Ghuba na Mashariki ya Kati ili kuongeza idadi ya watalii nchini na kukuza pato la Taifa kupitia sekta hiyo.
Ametoa kauli hiyo Jumatano, Desemba 17, 2014 wakati akizungumuza an waandishi wa habari mara baada ya kufungua Kongamano la siku mbili la Utalii na Uwekezaji lilionza leo kwenye hoteli ya Le Meridien, jijini Dubai, Falme za Kiarabu.
“Tunao mkakati wa kukuza utalii nchini lakini wengi wamekuwa wakitoka Ulaya na Marekani. Eneo ambalo tumeona tuwekeze kwa nguvu kwa maana ya kuongeza idadi ya watalii ni hili la nchi za ghuba na Mashariki ya Kati,” alisema.
Waziri Mkuu alisema kimahusiano Tanzania iko karibu na nchi hizi za ghuba lakini pia wanao uwezo wa kifedha wa kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ya utalii. “Amani ya nchi yetu ni kivutio kingine kikubwa cha uwekezaji, sisi tuko tayari kuwasaidia wafike huko tunakotaka,” alisema.
Alitoa wito kwa makampuni yanayotaka kuwekeza nchini yaangalie fursa zilizopo kwenye ujenzi wa hoteli za kawaida, hoteli za mahema (Tented Camps) na hoteli zenye kutoa huduma za vyakula (Special Cuisine Restaurant).
Hata hivyo, aliwataka wawekezaji watakaokuja wafanye juhudi ya kushirikiana na watanzania wazawa ili nao wajione ni sehemu ya uwekezaji huo.
Mapema, akifungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema katika kipindi cha miaka mitano, Tanzania imeweza kuongeza idaidi ya watalii kutoka 714,367 mwaka 2009 hadi kufikia watalii 1,095,884 kwa mwaka 2013.
“Kiwango cha mapato ya watalii hao kiliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.2 hadi kufikia dola za Marekani bilioni 1.8 katika kipindi hicho hicho cha miaka mitano,” alisema na kuongeza kuwa sekta hiyo inaajiri watu zaidi ya 400,000 kuchangia asilimia 17 kwenye pato la Taifa.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu akizungumza na washiriki wa kongamano hilo kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu alisema Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa kuhifadhi rasilmali zake na kuzitumia kwa utalii. “Nchi inayoongoza duniani ni Brazil,” alisema.
Akiainisha fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii nchini (TTB), Bi. Devothe Mdachi alisema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji kupitia sekta ya utalii zikiwemo uendelezaji wa fukwe, michezo ya majini na utalii wa mikutano (Conference Tourism).
“Kwenye kumbi za mikutano, Tanzania inahitaji kumbi kubwa zenye uwezo wa kuchukua watu kati ya 5,000 na 10,000 na hasa kwenye miji mikubwa kama Arusha, Dar es Salaam na Mwanza,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Bibi Julieth Kairuki aliwaeleza washiriki wa kongamano hilo kwamba utalii una fursa kubwa ya uwekezaji kama ilivyo kwenye sekta nyingine za madini na uchumbaji gesi.
“Uwekezaji hivi sasa umepanuka, na soko la utalii nchini Tanzania ni fursa kubwa sana ya kuwekeza. Tunawasihi watu wenye mitaji mikubwa waangalie fursa hiyo na kuichangamkia kama njia mojawapo ya kuwekeza nchini Tanzania,” alisema.