Idris Sultan ndio mshindi wa Big Brother Africa Hotshots. Baada ya kutupa karata yake kwa takriban miezi miwili ndani ya jumba hilo lililopo nchini Afrika Kusini, Afrika imemchagua kuwa mshindi wa msimu huo wa Big Brother na hivyo kushinda kitita cha $300,000 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 514 za Tanzania.
Idris ambaye ni mpiga picha katika kampuni ya I-View Studios, anarudi nyumbani kama milionea mwenye uwezo wa kuanzisha kampuni yake mwenyewe. Idris alionesha mapema kuwa mshindani mwenye nguvu na anayependwa zaidi katika shindano hilo na wengi walitabiri kuwa mshindi wa mwaka huu.
Maisha yake katika jumba hilo yalitawaliwa na ‘uplayboy’ kama alivyosema siku anaingia kwenye jumba hilo. Akiwa mjengoni, Idris alikuwa na uhusiano na wasichana wawili, Ellah wa Uganda na Goetse wa Botswana ambao wote waliondolewa pamoja wiki iliyopita. Pia alikuwa na urafiki wa karibu na Samantha kiasi cha kupewa jina la utani, Samdris.
Hiyo ilimfanya Idris kuonekana kama mzee wa totoz na hivyo kujipatia mashabiki wengi hususan wa kike barani Afrika.
Mastaa wa Afrika Mashariki na watu wengine waliungana kumpigia debe Mtanzania huyo ili ashinde shindano hilo baada ya kuwa mshiriki pekee kutoka Afrika Mashariki aliyesalia kwenye shindano hilo lenye mashabiki wengi.
Ushindi huo wa Idris, unaingozea Tanzania heshima kubwa katika tasnia ya burudani barani Afrika baada ya wiki iliyopita Diamond Platnumz kushinda tuzo tatu za Channel O.
Hii ni mara ya pili ushindi wa Big Brother Afrika unarejea Tanzania. November 2011, Richard Dyle Bezuidenhout aliibuka mshindi wa Big Brother Africa 2 baada ya kukaa mjengoni kwa siku 98 mfululizo. Richard alishinda US$100,000.