Mtu mmoja anayesadikiwa kuwa ni mganga wa kienyeji, anadaiwa kumbaka na kumwingilia kinyume na maumbile msichana mwenye umri wa miaka 19 aliyemsindikiza dada yake kwa mganga huyo kupata tiba.
Mganga huyo, Ali Abdulrahman Ali (45), anadaiwa kufanya kitendo hicho Novemba 26, mwaka huu, nyumbani kwake eneo la Kwamtipura Wilaya ya Mjini Unguja.

Mrakibu mwandamizi wa jeshi la polisi, kituo cha polisi Mwembemadema, Haji Abdallah Haji, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Alisema polisi inaendelea na upelelezi ambapo mtuhumiwa yupo nje kwa dhamana na upelelezi utakapokamilika jalada lake litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ili afikishwe mahakamani.

Daktari wa kitengo cha mkono kwa mkono katika Hospitali ya Mnazimmoja, Dk. Msafiri Marijani, ambaye alimpokea msichana huyo kwa uchunguzi, aligundua kuwa ameingiliwa katika sehemu zote za siri.

Muathirika wa tukio hilo (jina linahifadhiwa) alisema, Novemba 26, mwaka huu, alimsindikiza dada yake aliyekwenda kupatiwa tiba kwa mganga huyo na walipofika mganga aliwataka walale hadi siku ya pili ndio tiba itakuwa imekamilika.

Alisema ilipofika saa 7 usiku wakiwa wamelala, mganga huyo alimfuata kitandani kwake na kumfanyia kitendo hicho huku akimziba mdomo asipige kelele.

“Wakati tumelala mimi na dada chumba kimoja huku kila mtu akilala kwenye kitanda chake, nilishtuka kumuona mtu amenikalia juu kifuani huku akiniziba mdomo na kuniambia nikipiga kelele ataniua. Wakati huo dada alikuwa amelala hana habari,” alisema.

Mama wa mtoto huyo alisema mganga huyo amekuwa akimpatia tiba mtoto wake huyo mwenye matatizo ya akili.

Alisema baada ya kugundua mtoto wake amefanyiwa kitendo hicho, mtoto wake mwingine mwenye umri wa miaka 35 ambaye pia hupatiwa tiba na mganga huyo, alisema na yeye alikuwa anamfanyia kitendo hicho na kumwambia kuwa ndio tiba ya maradhi yake.

Mwandishi wa habari hizi alimtafuta mganga huyo kuzungumzia tuhuma hizo, lakini alikana na kusema kuwa huo ni uzushi. Hata hivyo alikiri wasichana hao kulala nyumbani kwake.

Mtuhumiwa huyo pia anadaiwa kumjeruhi mfanyakazi wake wa ndani kwa kumwagia maji ya moto baada ya kumkataa kimapenzi miezi minne iliyopita.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

 
Top