WATU watano wamekufa na wengine 36 kujeruhiwa baada ya lori walilokuwa wakisafiria kwenda msibani kupata hitilafu katika mfumo wa breki na kisha kutumbukia kwenye korongo.
Taarifa zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi zilieleza kuwa ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa nane mchana katika mteremko wa Kanyegele, Kata ya Ntokela wilayani Rungwe.

Kamanda Msangi alisema lori hilo aina ya Mitsubishi Fuso yenye namba za usajili T143 ACR lilikuwa likitokea Ilemi jijini Mbeya likiwa limebeba maiti na waombolezaji kuelekea wilayani Rungwe.

Alisema baada ya kufika katika mteremko wa Kanyegele dereva wa gari ambaye hakufahamika jina lake mara moja alipojaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake ghafla lilijitokeza gari jingine mbele yake na alipojaribu kuminya breki lilimshinda na hatimaye kutumbukia kwenye korongo na kusababisha vifo na majeruhi hao.

Alisema kati ya majeruhi 36, wawili walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kutokana na hali zao kuwa mbaya zaidi, tisa wakapelekwa hospitali ya Wilaya ya Rungwe ya Makandana na 25 walipelekwa katika kituo cha afya Igogwe.

 
Top