Mmoja wa akina mama aliyehuzunishwa na msiba huo |
Tukio hilo la kutisha lilijiri mwanzoni mwa mwezi huu, katika Kitongoji cha Kyawazaru Kata ya Kukirango wilayani Butiama, Mara.Licha ya kuchinjwa shingo, mwili wa marehemu huyo ulikutwa na majeraha kibao ikiwemo tumbo lake kupasuliwa na macho kutobolewa kwa kitu chenye ncha kali.
WACHINJAJI AKINA NANI?
Chanzo cha habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara zinasema, mwalimu huyo alichinjwa kikatili na watu wasiojulikana lakini awali alipigiwa simu na mwanafunzi wake mmoja wa kidato cha nne (jina tunalihifadhi kwa sasa), mwenye umri wa miaka 23 ambaye alitoweka na anatafutwa.
DAKIKA ZA MWISHO ZA UHAI WAKE Taarifa zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, ACP Alex Kalangi zinaelezea kwa kina jinsi mwalimu huyo alivyopita katika dakika za mwisho za uhai wake wa duniani.
Waombolezaji wakimfariji mama wa marehemu Alfred Ghozi msibani.
Inadaiwa Desemba 7, mwaka huu, saa 1:30, marehemu aliondoka Kiabakari akiaga kwa watu wake wa karibu kwamba anakwenda kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Kataryo uliopo kata hiyo baada ya kupigiwa simu na mwanafunzi huyo aliyekuwa akimdai shilingi 450,000.
“Kwa mujibu wa vyanzo vyetu ni kwamba mwanafunzi huyo alimpigia simu mwalimu wake aende mgodini ili akamlipe fedha alizokuwa akimdai.“Mwalimu huyo kwa vile alikuwa na safari ya kwenda kwao wilayani Ngara mkoani Kagera kwa likizo ya Desemba aliamua kuzifuata fedha hizo kama alivyaombiwa na mwanafunzi wake,” kilisema chanzo ndani ya jeshi la polisi.
MWALIMU AENDA KIMOJA
Habari zaidi zinasema, mara baada ya Mwalimu Ghozi kwenda kuitikia wito wa mwanafunzi wake ambaye pia anajishughulisha na uchimbaji wa dhahabu kipindi hiki cha likizo, hakurejea tena nyumbani kwake.
Ilipofika Desemba 9, mwaka huu, baadhi ya watu wake wa karibu walianza kujiuliza kisa cha mwalimu huyo kutorejea kwake lakini halikupatikana jibu la wazi.
Ndugu na jamaa wa karibu wakitoa heshima zao za mwisho kwa marehemu Alfred Ghozi.
Wapo waliokataa kuamini kwamba huenda alikutana na mkasa mzito njiani akienda au akirejea kwa vile mwalimu huyo hakuwa na tabia ya kumuwezesha kuwa na maadui.
WANANCHI WAKUSANYIKA
Baada ya kuona hali si ya kawaida, baadhi ya wananchi, wakiwemo bodaboda wa Kiabakari, walikusanyika wakiongozwa na wapanda pikipiki wa Kiabakari na kuelekea mgodini ambako mwalimu huyo aliaga anakwenda kufuata fedha zake.
Lakini wakiwa wanakaribia mgodini, walimkuta mwalimu huyo kichakani akiwa umechinjwa shingo, mwili wake umekatwakatwa sehemu mbalimbali hasa tumboni kiasi cha kuufanya utumbo kuwa nje.
MWANAFUNZI ATOROKA
Akiongoza waombolezaji katika shughuli ya kuuaga mwili wa mwalimu huyo, Desemba 10, mwaka huu katika Viwanja vya Shule Sekondari ya Kukirango, Mkuu wa Wilaya ya Bitiama, Angela Mabula alilaani mauaji hayo ya kinyama.
Marehemu Alfred Ghozi enzi za uhai wake.
Mabula akawataka wananchi kushirikiana na polisi kuwajua watu waliomchinja mwalimu huyo, akiwemo mwanafunzi huyo ambaye inaaminika alitumika kumuita marehemu kwa kumlaghai kuwa anataka kumlipa deni lake kumbe sivyo.
“Wahusika wote wa mauaji hayo akiwemo mwanafunzi wametoroka, hivyo kuwapa kazi polisi kuwasaka na kuwakamata ili wawafikishe kwenye vyombo vya sheria, mshirikiane nao,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Kamanda Kalangi aliyekiri kutokea tukio hilo, alisema hajakamatwa mtu yeyote kuhusiana na mauaji hayo lakini makachero wa polisi bado wapo kazini wakiendelea na msako.
Marehemu alizikwa nyumbani kwao Rulenge wilayani Ngara mkoani Kagera mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.
Chanzo Global