Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha
Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Suzana Luhende(60) mkazi wa kijiji cha Jomu kata ya Tinde wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga ameuawa kwa kupigwa na fimbo kichwani,usoni na miguuni na mme wake baada ya kutokea ugomvi kati yao kwa mme kumzuia mke wake kwenda kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika kote nchini Desemba 14 mwaka huu.
Tukio hilo limetokea Desemba 14 mwaka huu saa 11 jioni nyumbani kwao katika kitongoji cha Mwandu,kijiji cha Jomu kata ya Tinde ambapo Masanja Kapela(62) mkazi wa kijiji hicho alimpiga mke wake kwa fimbo hadi kufa.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kifo hicho kilitokana na ugomvi uliokuwepo kati yao baada ya mme ambaye ni mfuasi wa Chama Chama Mapinduzi kumkataza mkewe kwenda kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Mme alikuwa hataki mke wake apige kura kwa wagombea wa Chadema,hata hivyo wanandoa hao walikuwa wakigombana mara kwa mara kutokana na kwamba wote wanakunywa sana pombe za kienyeji”,alisema mmoja wa mashuhuda hao ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Jomu Cheyo Maganga alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa wakati tukio linatokea yeye alikuwa anafanya shughuli mbalimbali za uchaguzi.
“Tukio hili lipo,taarifa nilizonazo ni kwamba wanandoa hao walikuwa na ugomvi tangu Desemba 13,2014,wote hao ni wanywa pombe wazuri,siku hiyo mke alikwenda kunywa pombe na kumwacha mme wake kitendo kilichomkera mme naye akaenda kunywa pombe baada ya mke wake kurudi”,alisimulia afisa mtendaji wa kijiji cha Jomu.
“Kutokana na kutoelewana hukokwa taarifa nilizonazo huenda ndiko kulikomfanya mtuhumiwa kuanza kumpiga mke wake kutokana na kwamba pombe ilikuwa bado iko kichwani”,aliongeza Maganga.
Hata hivyo alisema hana uhakika kuhusu uvumi uliopo kuwa tukio hilo limetokana na itikadi za kisiasa kwamba mke alikatazwa kwenda kumpigia kura wagombea wa Chadema.
“Hizi taarifa za itikadi za kisiasa siyo za kweli,unajua tukio likitokea kila mtu anaibuka na jambo lake “,alisema Maganga.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha alisema chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana na uchunguzi unaendelea na kwamba mtuhumiwa alikimbia baada ya kusababisha mauaji hayo.
Credit: Malunde1 blog