Taarifa za mazishi ya mnenguaji maarufu kwenye familia ya muziki wa dansi Tanzania Aisha Mohamed Mbegu maarufu kama ‘Aisha Madinda’ zimeahirishwa kutokana na upelelezi wa Polisi unaoendelea juu ya kifo cha marehemu kwani kumekuwa na utata juu ya kifo cha mwanadada huyo kilivyotokea.
ALIYEKUWA mnenguaji na mwimbaji wa Bendi ya Twanga Pepeta, Aisha Madinda aliyefariki jana asubuhi, atazikwa kesho mchana badala ya leo kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali.

Mtoto wa kwanza marehemu, Feisal amesema kuwa polisi wamesema ni lazima mwili wa mama yake ufanyiwe upasuaji (postmortem) ili kujua chanzo cha kifo chake.

Awali ndugu wa marehemu walisema hawahitaji Asha Madinda afanyiwe upasuaji, lakini baada ya polisi kutembelea eneo la tukio la kifo chake huko Mabibo, wamesema ni lazima upasuaji ufanyike.

Feisal amesema upasuaji unatarajiwa kufanyika leo mchana hali inayowalazimisha kubadili ratiba ya mazishi. Aisha Madinda sasa atazikwa kesho mchana baada ya sala ya Ijumaa.

 
Top