Mheshimiwa Hebert Mtangi kushoto akiwa kazini.

Stori: Abdallah Juma, Muheza
Muheza ni moja kati ya wilaya nane zinazounda Mkoa wa Tanga. Kwa upande wa Kaskazini, Muheza inapakana na nchi ya Kenya, upande wa Mashariki kuna Jiji la Tanga na Bahari ya Hindi, Kusini inapakana na Wilaya ya Pangani wakati Magharibi kuna wilaya za Lushoto na Korogwe.

Pia Muheza ni Jimbo la uchaguzi lenye jumla ya kata 37, likiongozwa na Mheshimiwa Hebert Mtangi kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wiki iliyopita, Gazeti la Uwazi lilichanja mbuga mpaka kwenye jimbo hilo na kufanikiwa kuzungumza na wananchi wa baadhi ya kata za Majengo, Masuguru, Mbaramo, Magoroto, Magila, Bwembwera, Manza, Duga, Gombero, Maramba na nyingine nyingi.
Eneo la Muheza, Tanga.

Katika ziara hiyo, Uwazi lilizungumza na wananchi ambao walieleza kero mbalimbali zinazowasumbua, kubwa ikiwa ni kutokamilika kwa miradi mingi iliyoahidiwa na Mbunge Mtangi wakati wa kampeni.

MATATIZO YA WANANCHI NA MAJIBU YA MBUNGE
Abdul Shaban, mkazi wa eneo la Mbaramo, Muheza Mjini yeye alianza kwa kumpongeza mbunge wake kwa kutimia kwa ahadi ya kukifufua Kituo cha Afya cha Ubwari lakini akahoji:

“Wakati wa ziara ya Rais Kikwete wilayani hapa alipohutubia wananchi katika Uwanja wa Jitegemee, kwa pamoja mliahidi kutuletea gari la kubebea wagonjwa (ambulance). Mbona halijawasili mpaka leo wakati mnaelekea kumaliza muda wenu wa uongozi?”

Jibu: Ahsante kwa pongezi, ni kweli Kituo cha Afya cha Ubwari kimekamilika, tulikuwa tunasubiri ujenzi wa majengo ya sehemu ya kufulia na kuchoma takataka ambayo yamekamilika na sasa kituo kinafanya kazi. Kuhusu ambulance ya kubebea wagonjwa, mheshimiwa rais ameahidi kuwa kabla ya kumaliza kipindi chake cha uongozi itakuwa imeshawasili kwa hiyo msiwe na wasiwasi.

Naye Rose Alphonce, mkazi wa Genge, Muheza alikuwa na swali lifuatalo kwa mheshimiwa mbunge:

“Mheshimiwa mbunge, katika ahadi zako wakati unagombea ubunge, wewe pamoja na Rais Kikwete mliahidi kulipatia ufumbuzi tatizo la uhaba wa maji jimboni kwetu ambalo limekuwa likitutesa wananchi kwa muda mrefu. Mlisema mtaleta maji kutoka chanzo cha Mto Zigi, mbona mpaka muda huu mmebakisha mwaka mmoja hakuna dalili yoyote ya ufumbuzi wa tatizo hili?”

Jibu: Kuhusu mradi wa kuleta maji kutoka Mto Zigi mpaka Muheza, 

mheshimiwa rais amesema kuwa mradi huo pamoja na ule wa Karagwe mkoani Kagera ni moja ya miradi mikubwa ambayo inahitaji fedha nyingi hivyo serikali yake inafanya mazungumzo na wahisani mbalimbali na ameahidi wananchi katika ziara yake wilayani hapa kuwa analifanyia kazi. Ameahidi hata kama siyo yeye hata rais ajaye atamfahamisha ili likamilike.

“Mheshimiwa mbunge, katika ahadi zako uliahidi kuijenga Barabara ya Muheza-Amani kwa kiwango cha lami lakini mbona mpaka muda huu hiyo barabara katika kiwango cha lami imeishia eneo la Msangazi hapohapo Muheza? Amani itafika lini?” hilo ni swali kutoka kwa Juma Shemdoe, mkazi wa Zirai, Amani.

Jibu: Kuhusu Barabara ya Amani, ujenzi wake unaendelea awamu kwa awamu lakini barabara hiyo huwa inafanyiwa marekebisho ya mara kwa mara katika maeneo korofi na Tanroads.

“Mheshimiwa mbunge, naitwa Ally Mdoe, mkazi wa Muheza. Uliahidi kuwapatia ardhi ya kulima wananchi wa Muheza kwa kubadili hati za mashamba ya mkonge ya Kibaranga na Muheza Estate, mbona mpaka leo unakaribia kumaliza kipindi chako hatuoni chochote?

Jibu: Ugawaji wa ardhi katika mashamba ya mkonge ya Kibaranga na Muheza upo katika hatua nzuri, wananchi wasiwe na wasiwasi ardhi itapatikana bila ya tatizo lolote.

“Sisi wakazi wa Amani ambao tumehamishwa kwa kupisha hifadhi ya msitu wa asili wa Amani wengine mpaka leo tunadai stahiki zetu na serikali inatuzungusha. Je, ni lini tutalipwa?
Jibu: Serikali inalifanyia kazi hilo suala na kila mtu atapata haki zake bila ya tatizo.

 
Top