Sitti Mtemvu Katikati akiwa na washindi wenzake katika shindano la mwaka 2014
Shindano la Miss Tanzania limesimamishwa kwa muda wa misimu miwili ili kutoa fursa kwa waandaaji wa shindano hilo kurekebisha baadhi ya kasoro ambazo zimekuwa zikilalamikiwa mara kwa mara.
Akizungumza na EATV Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa Godfrey Mngereza amesema kuwa serikali kupitia baraza hilo imefikia umamuzi huo kutokana na malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wadau mbalimbali na wapenzi wa shindano hilo.

Amesema imefika wakati sasa waandaji warekebishe masuala kadha ili kuondoa malalamiko na manung'uniko miongoni mwa wadau ili kulipa heshima shindano hilo, pia liweze kuheshimika na kila mtu.

Mngereza ameongeza kuwa, serikali kupitia wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imelipa dhamana baraza hilo kisheria kushughulikia masuala yote yanahusu sanaa na Utamaduni hivyo baraza hilo lina mamlaka ya kuingilia kati endapo litajiridhisha kuwa kuna masuala hayaendi sawasawa.

Kuhusu masuala wanayotakiwa kuyarekebisha, Mngereza amesema kuna mambo mengi hayako sawa katika mchakato mzima kuanzia katika ngazi ya vitongoji, na baraza limekuwa likipata malalamiko karibu kila mwaka lakini kwa mwaka huu malalamiko yamekuwa mengi zaidi.

Mngereza amesema “Kama imefikia wakati hadi mshindi wa shindano mwenyewe analazimika kuvua taji lake kwa shinikizo, ina maana kuna tatizo, kwahiyo tumewapa muda ili wakaangalie upya mchakato mzima na wafanye marekebisho”

Kuhusiana na sakata la umri wa aliyeshinda shindano hilo kwa mwaka 2014 Sitti Mtemvu, Mngereza amesema kuwa suala la kuthibitisha umri wa mrembo huyo linafanyiwa kazi na Mamlaka husika ambayo ni RITA, na kwamba BASATA haihusiki nalo kabisa.

Amemalizia kwa kusema kuwa mrembo Lilian Kamazima aliyetwaa taji hilo baada ya kuvuliwa na Sitti Mtemvu ataendelea kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia kwa mwaka 2015 kama ilivyopangwa, lakini hakutakuwa na mashindano mengine kwa kipindi cha miaka miwili ndani ya Tanzania kuanzia ngazi ya vitongoji.


 
Top