Askari wa zimamoto akishuhudia nyumba ilivyoteketea kwa moto.
KATIKA hali isiyo ya kawaida, nyumba ya mkazi wa Kata ya Nyasho Manispaa ya Musoma, David Obambo, imeungua moto mara tatu ndani ya mwezi mmoja na kuwashangaza watu.
Tukio la kwanza la kuungua kwa nyumba hiyo, lilitokea Desemba 10, mwaka huu saa 7 mchana na wiki moja baadaye siku kama hiyo na muda huo nyumba hiyo iliungua tena na kusababisha baadhi ya watu kuhusisha kuungua nyumba hiyo na imani za ushirikina.
Mara ya tatu kuungua kwa nyumba hiyo ilikuwa Desema 18 mwaka huu, jambo ambalo limeendelea kuwashangaza wengi huku baadhi ya marafiki wa mwenye nyumba wakishauri nyumba hiyo isikaliwe kwa sasa na kutafuta namna ikiwemo ya kufanya maombi ili tatizo la moto kwenye nyumba hiyo liweze kuondoka.
Wakizungumza na gazeti hili kwenye eneo la tukio, baadhi ya majirani walidai kuwa ni lazima kutakuwa na imani za ushirikina kwani tukio la tatu umeme ulikuwa umeshatolewa kwenye nyumba hiyo lakini ulitokea mlipuko wa moto.
Mmiliki wa nyumba hiyo Bw. David Obambo akisema anachofahamu juu ya janga hilo.
Mmoja wa majirani na mashuhuda wa matukio yote matatu ya kuungua kwa nyumba hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Mutoka Mukebezi, alisema: “Hapa kuna namna na haya mambo ya kishirikina yapo, natoa ushauri wajaribu kuangalia kwa undani suala hili kama hali hii ikiendelea huenda siku moja moto ukalipuka usiku na kupoteza uhai wa watu.”
Mmoja wa wanafamilia katika nyumba hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Bahati Obambo alisema hawezi kulisemea suala hilo na imani za kishirikina moja kwa moja lakini wameshangazwa na matukio matatu ya kuungua kwa nyumba hiyo na kuteketeza thamani za ndani pamoja na vyakula.
Kwa upande wake mmiliki wa nyumba hiyo David Obambo, alisema anachofahamu kuungua kwa nyumba hiyo ni tatizo la umeme na alishalitolea taarifa Tanesco mara baada ya siku ya kwanza ya tukio lakini hakuna jibu ambalo amepewa hadi sasa.