NI AIBU! Ndivyo unavyoweza kushangaa baada ya mtu mmoja anayedhaniwa kuwa ni askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kunywa pombe kiasi cha kupoteza fahamu akiwa na sare za taasisi hiyo inayoheshimika nchini na kujikuta akilala karibu na mtaro, katika stendi kuu ya mabasi mjini Iringa.
 
Anayedhaniwa kuwa mwananjeshi akiwa amelala kwenye mtaro.

Habari kutoka eneo la tukio zinasema mtu huyo alipanda basi liitwalo Mgumba huko Mafinga, ambako ipo kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambalo lilikuwa likielekea mjini Iringa. Abiria waliokuwa pamoja naye garini,

wanaripoti kuwa akiwa humo, tayari akionekana amelewa, aliendelea kunywa pombe kali inayokaa kwenye pakiti, maarufu kama viroba.

Akisimulia zaidi, mmoja wa abiria wa basi hilo alisema akiwa bado anaendelea kunywa, ghafla alianza kutapika na kujisaidia haja ndogo kiasi cha kuwachefua watu wengine.“Tulipofika stendi, tukalazimika kumsaidia kumshusha huku akiwa hajitambui kabisa. Akalala mtaroni, ikabidi tummwagie maji, ndipo alipozinduka na kupata fahamu kidogo.
 
Baadhi ya watu wakimshangaa mwanajeshi huyo.

Alikuwa anaona aibu sana, akajikakamua na kutoa namba ya simu ya rafiki yake, ambaye ni askari wa FFU mjini Iringa, ambaye alipigiwa na kuja kumnusuru,” alisema abiria huyo aliyekataa kutaja jina lake.

Gazeti hili liliwasiliana na kiongozi mmoja wa kambi ya Jeshi Mafinga, ambaye baada ya kuelezwa kuhusu askari huyo, alikiri kuwa ni mwenzao, lakini siyo wa kambi hiyo.

“Ni kweli nimeziona hizo picha, huyo jamaa kweli ni askari mwenzetu lakini siyo wa kambi hii, huyo anatoka Itende, Mbeya. Jaribu kuwasiliana nao kule wanaweza kukupatia taarifa maana sisi tulishawataarifu,” alisema kiongozi huyo, aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa vile siyo msemaji wa Jeshi.

Juhudi za kumpata Mkuu wa Kikosi cha Itende hazikuweza kufanikiwa, lakini Kaimu Msemaji wa Jeshi la Wananchi, Makao Makuu Dar es Salaam, Meja Joseph Masanja, alipatikana na yeye kukiri kuziona picha hizo mitandaoni.

“Ni kweli nimeziona picha hizo na ninazo hapa, lakini kama unavyoziona, kuna gizagiza kiasi kwamba huwezi kumtambua. Ni vigumu kusema huyo ni askari wetu kwa sababu picha haionekani, huenda ni mtu tu kalewa akiwa na nguo za jeshi.
 
Mkuu wa majeshi Davis Mwamunyange.

Alipoulizwa kuhusu adhabu anayoweza kupata endapo atafahamika kuwa ni mwanajeshi, Masanja alisema hayo ni masuala ya utawala yanayotofautisha makosa ya kijinai na nidhamu.

“Vilevile inakuwa vigumu kidogo kujua kwa nini mtu aliyepiga picha aliamua kuposti kwenye mitandao,” alisema Meja Masanja akisisitiza Jeshi bado linaendelea kutafuta ukweli wa picha hizo.

 
Top