Wagombea 68 wa nafasi mbalimbali za uongozi katika jimbo la Arumeru Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamewekewa pingamizi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kutotimiza vigezo na masharti ya tume ya uchaguzi.
Baadhi ya wagombea hao waliowekewa pingamizi wa CHADEMA wametafsiri hali hiyo kama njama za kisiasa zinazofanywa na chama tawala kutaka kuwaathiri kisaikolojia na wamesema baadhi ya watendaji wa vijiji wanachangia kuwepo kwa hali hiyo.
Baadhi ya viongozi wa chama hicho akiwemo mbunge wa jimbo hilo Mh Joshua Nassari wameziomba ngazi zinazohusika kushughulikia suala hilo kabla halijaleta madhara kwani kuendelea kulifumbia macho ni kutengeneza matatizo yasiyo ya lazima.
Akizungumzia malalamiko hayo katibu tawala wa wilaya ya Arumeru Bi Boma amesema wanaendelea kusimamia zoezi hilo kwa mujibu wa sheria na maelekezo ya tume na kwamba wote wanahisi kuwa hawajatendewa haki, wana haki ya kukata rufaa.
Chanzo:EATV