Polisi wakiwa eneo la tukio.Stori Mwandishi Wetu, Mwanza
Roho mkononi! Jumla ya magari saba yakiwemo mabasi mawili yaliyokuwa yakitokea jijini Dar es Salaam kuelekea Mwanza, yametekwa na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi usiku wa kuamkia Jumamosi ya wiki iliyopita, saa 6:30 usiku eneo la Ng’ungumalwa mkoani Mwanza. 
Miongoni mwa magari yaliyotekwa, mawili yalikuwa ni mabasi ya abiria, Super Najmnisa na Princess Mnaa huku mengine yakiwa ni malori na gari dogo moja ambapo inaelezwa kuwa watekaji walitegesha mawe makubwa barabarani kabla ya kutekeleza tukio hilo.
Wakizungumza na mwandishi wetu aliyekuwepo eneo la tukio, baadhi ya madereva wa magari yaliyotekwa walieleza kwamba walipofika eneo hilo, walikuta mawe yakiwa yametegeshwa barabarani huku kukiwa na kundi la watu wenye silaha za aina mbalimbali yakiwemo mapanga, marungu na bunduki.

Baadhi ya abiria waliotekwa. “Walitushusha kwenye magari na kututaka tusalimishe kila kitu tulichokuwa nacho zikiwemo fedha na simu za mkononi. Waliokuwa wakionesha ukaidi walikuwa wakipigwa na kujeruhiwa vibaya,” alisema dereva mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Madereva hao waliendelea kueleza kuwa kazi hiyo ya utekaji iliendelea kwa takribani saa nzima ambapo kila gari lililokuwa likija eneo hilo, lilikuwa likitekwa na watu kulazimishwa kushuka chini na kutoa kila walichokuwa nacho.
Msichana huyu alizimia baada ya kutekwa.
 “Walikuwa na mifuko mikubwa miwili, mmoja ulijaa simu walizotupora na mwingine ulijaa fedha, kwa kweli lilikuwa ni tukio baya sana, wengi walijeruhiwa vibaya,” alisema dereva mwingine ambaye naye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Abiria wengine waliozungumza na Uwazi, walienda mbele zaidi kwa kueleza kuwa mbali na kupigwa na kuporwa, pia baadhi ya abiria wanawake walibakwa na kusababishiwa maumivu makali.
“Huu unyama tuliyofanyiwa wa kupigwa na kuporwa mali zetu huku baadhi yetu wakibakwa unatisha sana na unaonesha ni kwa jinsi gani nchi inaelekea kubaya, hakuna amani hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya,” alisema mwanamke mmoja aliyekuwa miongoni mwa waliotekwa, aliyejitambulisha kwa jina moja la Sara.
Abiria wakiwa wameduwaa 
Abiria hao waliliambia Uwazi kwamba eneo hilo lina pori kubwa ambapo panahitajika doria za mara kwa mara za polisi kwani ni eneo ambalo limekuwa maficho ya majambazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alipopigiwa simu na kuulizwa juu ya tukio hilo, alikiri kuwa na taarifa na kueleza kuwa polisi walifika katika eneo la tukio muda mfupi baadaye baada ya kupata taarifa na kufungua barabara iliyokuwa imefungwa na kuruhusu magari kupita.“Msako mkali unaendelea kuwatafuta watuhumiwa katika Wilaya ya Kishapu na Kwimba,” alisema Kamanda Mlowola.

 
Top