MWALIMU wa Shule ya Sekondari Mazungwe, Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma, amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma, Maweni, kwa ajili ya matibabu baada ya kuungua vibaya na moto wa gesi.
Revania Ndabigeze, mwenye umri wa miaka 39, mkazi wa Mwandiga, Wilaya ya Kigoma, aliungua na moto wa gesi Jumanne iliyopita Disemba 9 majira ya saa tano asubuhi, wakati alipokuwa katika shughuli za mapishi nyumbani kwake.
Akielezea tukio hilo mwalimu huyo alisema kuwa siku ya Jumatatu alitoka kituo chake cha kazi kwenda kununua gesi mjini Kigoma na kwamba alipotaka kuunganisha na jiko ili aweze kutumia alishindwa na kumuita mwalimu mwenzake aitwaye Yusuf ili amsaidie ambaye hata hivyo hakufanikiwa.
“baadaye niliamua kujaribu tena mwenyewe kulingana na maelekezo niliyokuwa nimepewa wakati nanunua likakubali lakini haikupita dakika tano nikasikia harufu Fulani na nilipokwenda kuzima likaripuka na kuniunguza,”alisema.
Alisema baada ya tukio hilo alipelekwa Zahanati ya Mazungwe ambapo alipatiwa rufaa kwenda hospitali ya Maweni, Kigoma alipolazwa mpaka sasa kwa ajili ya matibabu.
Sehemu alizoungua mwalimu huyo ni usoni, shingoni, mabega, mikono yote miwili na miguu yote miwili, ambapo Daktari wa zamu Fadhili Kabaya, alisema kuwa hali yake inaendelea vizuri.
Mtaalam na Wakala ya Mitungi ya Gesi ya Kampuni ya ORYX, Issa Mangapi, alisema kwa kawaida kabla ya kuuza mitungi ya gesi kwa wateja hutoa elimu na tahadhari juu ya matumizi ya gesi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
Alisema gesi ni nishati muhimu bali watumiaji wanatakiwa kuwa waangalifu na kufuata na kuzingatia maelekezo ya wataalam ili kuepuka ajali ya moto kutokea kama ambavyo wanachukua tahadhari kwa vitu vingine kama vile umeme.
Na E.Matinde