Hali ya sintofahamu imeibuka katika mtaa wa Azimio, kata ya Kihonda katika manispaa ya Morogoro, baada ya mwanamke mmoja, Veronica Madebe, kukutwa akitaka kumtumbukiza mwanaye wa kiume ambaye ni pacha, mwenye umri wa kati ya miaka mitano hadi saba kwenye kisima cha maji, kutokana na kinachosadikiwa kuwa ni imani za kishirikina.
Tukio hilo limejiri katika eneo hilo la Azimio, baada ya mwanamke huyo kukutwa na mmiliki wa nyumba kilipo kisima hicho, Dani Haji, akijaribu kumtumbukiza kisimani mmoja wa watoto wake pacha, kwa madai yaliyoelezwa huenda ni kupungukiwa akili, ama ni imani za kishirikina.

Amedai kutumwa na wakazi wawili wa eneo hilo kufanya hivyo, na wakati mwingine kudai alikuwa kwenye kifungo na alipaswa kutoa kafara ya mtoto wake kwa kumtupa kisimani ili afunguke baada ya kuokoka kiimani, jambo lililothibitishwa pia na mmoja wa wajumbe wa serikali za mitaa katika eneo hilo.

Mmoja wa familia iliyotajwa na mwanamke huyo kufanya kitendo hicho cha kikatili, kilichozuiwa na wasamaria wema, anakiri kumfahamu mwanamke huyo lakini bila kuwa na matatizo yeyote, na alishangazwa na hatua hiyo na alipomuona aliamua kumvaa yeye na mtoto aliyekuwa amembeba, bila sababu zozote, hadi alipoamuliwa na kundi la wananchi waliojitokeza.

Wananchi wa eneo hilo walipigasimu polisi kuomba msaada wa dharura na kumpeleka mama huyo katika ofisi za mtendaji wa kata ya Kihonda, ambako ulinzi mkali wa polisi uliimarishwa, na baada ya muda mwanamke huyo alitolewa na kuingizwa kwenye gari ndogo kwa nia ya kupelekwa polisi, lakini alifanya vurugu hadi polisi walipoingilia kati na kumpakiza kwenye difenda na kuondoka naye.

 
Top