Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda.

Serikali imesema kasoro zilizotokea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa jana katika maeneo mbalimbali ya Tanzania hazikuathiri uchaguzi huo kwa sababu maeneo mengi ulifanyika kwa ufanisi.
Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Khalist Luanda, wakati akizungumza na NIPASHE kuhusu kasoro hizo.

Luanda alisema kasoro hizo zilizosababisha baadhi ya maeneo kuahirisha uchaguzi, haziepukiki kutokana na ukubwa wa uchaguzi huo, ambao aliutofautisha na ule wa madiwani, wabunge na urais.

“Kutokana na ukubwa wa uchaguzi, nathubutu kusema kasoro zilizojitokeza ni vigumu kuziepuka, hapa tunazungumzia vitongoji elfu 64, mitaa elfu 30 na vijiji elfu 13 tofauti uchaguzi wa wabunge takribani 300,” alieleza Luanda.

Kwa mujibu wa Luanda, Wilaya nzima ya Kaliua mkoani Tabora, uchaguzi uliahirishwa kwa sababu mbalimbali mpaka Jumapili ijayo.

Alisema hatua ya wasimamizi wa uchaguzi kuahirisha chaguzi kwenye maeneo yao, ni kwa mujibu wa kanuni ambazo zinaelekeza ufanyike tena, ndani ya muda usiyozidi siku saba.

Alitaja maeneo mengine ambayo kwa wakati huo alikuwa na taarifa kwamba uchaguzi uliahirishwa, kuwa ni Kata ya Dodoma Makulu, Mtaa wa Njedengwa – West.

Maeneo mengine yaliyokumbwa na kasoro mbalimbali kiasi cha kusababisha uchaguzi huo kuahirishwa, yalitajwa na Luanda kuwa ni pamoja na baadhi ya maeneo wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, hakueleza sababu za kucheleweshwa kwa vifaa wakati wiki iliyopita alisema maandalizi yalikuwa yamekamilika kwa asilimia 100.

Chanzo:-NIPASHE

 
Top