WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, wamesema baada ya hukumu ya Bunge sasa wanasubiri neno la Rais.
Viongozi hao waliyasema hayo jana, ikiwa ni siku chache tangu Bunge kupendekeza mamlaka za uteuzi ziwavue madaraka.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyowasilishwa bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ilionyesha viongozi hao walifanya makosa kadhaa na kusababisha uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Viongozi wengine ambao mamlaka zao za uteuzi zilitakiwa kuwavua nyadhifa zao ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye aliingiziwa Sh bilioni 1.6, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Sh bilioni 1.6 na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja Sh milioni 40.
Profesa Muhongo alisema: “Sina maoni, sasa wewe unataka kujua nini… kwani wewe umeonaje na ni lazima nikujibu au unataka nikujibu porojo… sasa nakujibu kwamba kaulize Bunge kuhusu hilo suala la Escrow na kama una maswali kuhusu mambo ya umeme nenda Tanesco watakujibu.”
Jaji Werema: Siwezi kubishana na Bunge
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, alisema hana kauli wala maoni yoyote na hawezi kubishana na Bunge.
“Siwezi kubishana na Bunge kwa sababu wenye mamlaka wamepewa kazi kuchukua hatua, acha wafanye kazi, au unataka nisemeje tena?” alihoji Jaji Werema.
Hatima ya Askofu Kilaini, Nzigilwa
Kanisa Katoliki nchini limesema haliwezi kuwaadhibu maaskofu wake waliotajwa kuingiziwa fedha zilizotokana na kashfa hiyo kwa sababu wanawajibika kwa kiongozi wa kanisa hilo duniani, Papa Francis.
Maaskofu wa kanisa hilo waliotajwa kwenye kashfa hiyo ni Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini aliyedaiwa kupewa Sh milioni 80.5 na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, Sh milioni 40.4.
Akizungumza na waandishi wa habari hizi jana, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki (TEC), Askofu Severin Niwemugizi, alisema hadi sasa hawajataarifiwa kama kuna kosa limefanyika, hivyo hawawezi kukutana.
“Kama kungekuwa na kosa angetaarifiwa rais wa baraza… kwakuwa hakuna kosa hakuna dharura yoyote ya kusema tukutane.
“Kama kanisa hatuna sababu ya kusema tuhamaki tuwaadhibu kwa sababu askofu yuko chini ya baba mtakatifu,” alisema Askofu Niwemugizi.
Hata hivyo, alisema kama vyombo vya dola vikifanya uchunguzi na kubaini kuna makosa ya kinidhamu au kijinai, hapo ndipo wanaweza kuchukua hatua.
“’Unless’ uchunguzi ukifanywa wakasema kuna makosa ya kijinai na kinidhamu taratibu nyingine zinaweza zikachukuliwa.
“Jambo hili linazungumzwa kisiasa zaidi na ukweli haukusemwa bungeni… hizi ni mbio za urais, sasa wanataka kuwaingiza na wengine ambao hawahusiki,” alisema.
Kuhusu Benki ya Biashara ya Mkombozi ambayo ilihusika kupitisha fedha hizo, Askofu Niwemugizi alisema ilifuata taratibu zinazotakiwa ndiyo maana walienda Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kujiridhisha.
“Benki inafanya biashara, na mteja anapoleta fedha wanafuata taratibu zinazotakiwa, benki nyingine ziliona wivu kwa kukosa hizo fedha na ndio wanaochochea,” alisema.
CAG mpya kuipitia Ripoti ya IPTL
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Musa Juma Asaad, amesema kazi yake ya kwanza ni kuipitia tena ripoti ya ofisi yake juu ya Akaunti ya Tegeta Escrow iliyojadiliwa bungeni hivi karibuni.
Profesa Asaad aliyasema hayo baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam jana.
“Nikianza kazi nitaipitia ripoti ya IPTL ambayo ilizua mjadala mkubwa katika Bunge hivi karibuni kwa sababu sijui kilichoandikwa, lakini nikiisoma na kutumia uzoefu wangu nitaweza kujua kinachoendelea,” alisema Asaad.
Alisema pia atafanya kazi kwa uadilifu na uaminifu ili kuhakikisha anatenda haki kwa kila atakayehusishwa na ripoti ili Serikali iweze kuchukua uamuzi.
“Siwezi kumuonea mtu, bali nitafanya kazi kwa uadilifu ili kuhakikisha kuwa natenda haki kwa kila mmoja, kwa sababu nina uzoefu wa mambo hayo, hivyo basi nitahakikisha haki inatendeka.
“Hii ni dhamana kubwa kwangu niliyopewa na rais, siwezi kumwangusha, hivyo basi nitahakikisha natimiza majukumu yangu kwa mujibu wa sheria ili ripoti zote ziwe na kiwango,” alisema.
Christopher Ole Sendeka
Siku chache baada ya Bunge kupitisha maazimio nane kuhusu kashfa ya Escrow, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), ameibuka na kusema baadhi ya wabunge walipokea rushwa ili kupoza mjadala bungeni.
Alisema rushwa ilivyokuwa inagawiwa kama njugu mjini Dodoma ilisababisha baadhi ya wabunge kutetea hoja za kuwalinda watuhumiwa jambo ambalo halikuwa sawa.
Akizungumza nakwa njia ya simu, Sendeka ambaye anafahamika kwa misimamo yake, alisema baadhi ya wabunge ambao waliipinga ripoti ya CAG na ile ya PAC hawakuwa na nia njema.
Baadhi ya wabunge waliokuwa vinara wa kutetea watuhumiwa na kupinga ripoti hiyo ni pamoja na Mbunge wa Kishapu, Suleiman Nchambi, Asumpta Mshama (Nkenge), Livingstone Lusinde (Mtera) na Richard Ndassa (Sumve) wote kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia.
Ole Sendeka alisema pamoja na kwamba hana ushahidi wa kimahakama, lakini kulikuwa na dalili za wazi za kuwapo vitendo vya rushwa kutolewa kwa baadhi ya wabunge.
“Siwezi kuwa na ushahidi wa kimahakama, lakini kulikuwa na dalili za wazi za rushwa kutolewa nje nje bila aibu na ndiyo maana ulishuhudia namna wengi walivyokuwa hawataki kuona ukweli ukisemwa na wakati mwingine kuwatetea mafisadi huku wakiwatupia kashfa wengine,” alisema Sendeka.
Alisema ni jambo lililo dhahiri kwamba kulikuwa na rushwa kutokana na baadhi ya wabunge kubadili misimamo yao ya awali.
“Hata wale ambao kawaida yao walikuwa na misimamo katika mambo ya msingi na taifa kwa ujumla, walibadilika ghafla jambo lililotushangaza na hilo lilituaminisha kwamba kulikuwa na rushwa ilitolewa kwa sababu haiwezekani mtu kutetea vitu ambavyo viko wazi,” alisema.
Taarifa hii imeandaliwa na Nora Damian, Patricia Kimelemeta na Elizabeth Hombo