Askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji akishuka baada ya kumuokoa mtoto eneo la Mabatini, jijini Mwanza lililokumbwa na mafuriko baada ya Mto Mirongo kufurika kutokana na mvua iliyonyesha jana. Picha na Michael Jamson
MVUA kubwa inayoendelea kunyesha mkoani Mwanza, imesababisha maafa makubwa yakiwamo ya watu kukosa sehemu za kujihifadhi, mitaa mingi kujaa maji na kukwamisha shughuli zote za kijamii.
Hali ilikuwa mbaya zaidi wilayani Kwimba ambako mafuriko yalionekana kuhatarisha maisha ya watu na mali zao.
Kutokana na Mvua hiyo iliyoanza kunyesha jana asubuhi, Mto Mirongo ulifurika na kusababisha mafuriko katika Mtaa wa Mabatini, hivyo magari kushindwa kupita eneo la Mlango Mmoja.
Akizungumzia hali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mulowola, alisema hadi saa 8 mchana hakukuwa na taarifa yoyote ya kuwapo vifo.
“Ninachoweza kusema ni kuwa mafuriko hayo yametokea na baadhi ya nyumba zimeathirika, lakini hatuna taarifa ya watu kupoteza maisha yao,” alisema.
Alisema mafuriko hayo yamesababisha nyumba nyingi kubaki tupu kutokana na vilivyokuwamo kusombwa na maji.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilifika eneo la tukio na kulazimika kuokoa baadhi ya wakazi waliokuwa wamekwama kwenye nyumba zao, huku wengine wakiwa juu ya paa.
Akizungumzia uokoaji huo, Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Masoud Gadafi, alisema walifanikiwa kuokoa watu zaidi ya 15 waliokuwa wamekwama ndani ya nyumba zao.
“Kazi ya uokoaji imefanyika vizuri, tunashukuru wenzetu wa Tanesco waliwahi kukata umeme mapema vinginevyo madhara yangekuwa makubwa,” alisema Gadafi.
Habari zaidi zinasema katika Wilaya ya Kwimba, watu zaidi ya 220 wa Kijiji cha Mwambayanda hawana mahali pa kuishi baada ya paa za nyumba 40 kuezuliwa na upepo mkali.
Akizungumza na wananchi hao jana, Diwani wa Kata ya Kikubiji, Sospeter Mhagija, alisema licha ya nyumba hizo kuezuliwa na nyingine kuanguka, pia chakula kilichokuwa kimehifadhiwa ndani ya nyumba na kwenye maghala kimeharibiwa.
“Wananchi hawana mahala pa kuishi, tunaomba ndugu, rafiki na majirani tusaidiane kuwahifadhi wenzetu wakati Serikali inaandaa taratibu nyingine,” alisema.
Jitihada za kuwapata Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Suleiman Mzee na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Pendo Malebeja hazikufanikiwa kutokana na simu zao za kiganjani kutokuwa hewani.
NA
BENJAMIN MASESE NA ABUBAKARI AKIDA, MWANZA