Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza
Watu tisa wanadaiwa kuuawa katika mapigano baina ya jamii za wafugaji wa kabila la Wabarbaig maarufu kama Wamang’ati na wasukuma wilayani hapa, mkoa wa Pwani.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Ulrich Matei, alithibitisha kutokea kwa mapigano hayo katika kijiji cha Kihale katikaTarafa ya Chole.
Matei alisema kuwa chanzo chake ni mgogoro ulioanza Novemba 26, mwaka huu baada ya mfugaji jamii ya Wamang’ati kutuhumiwa kuiba ng’ombe zaidi ya watano wa mfugaji wa Kisukuma.
Alisema baada ya wizi huo kutokea, vijana wa Kisukuma walianza msako na walipogundua aliyewaibia ng’ombe hao walimkamata na kumshambulia kwa kipigo hadi kufa.
Kamanda huyo alisema mauaji hayo yalichochea hasira kwa wafugaji wa Kibarbaig na kuamua kulipiza kisasi.
Alisema kitendo hicho kilisababisha kuibuka kwa mapigano hayo baada ya wafugaji wa Kisukuma kutokubaliana na kusababisha madhara zaidi vikiwano vifo hivyo.
Matei alisema miili mitano imekutwa imetupwa misituni na mashambani na mingine minne haijajulikana ilipo.Alisema uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini majina ya watu waliouawa na kuwasaka wauaji.
Alisema ataendelea kutoa taarifa zaidi kulingana na uchunguzi wa tukio hilounaoendelea.
Mkuu wa mkoa huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mwantumu Mahiza, alieleza kusikitishwa na mauaji hayo.
Mahiza aliliagiza Jeshi la Polisi kufanya msako mkali kuwakamata waliohusika na mauaji hayo na kuhakikisha wanafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Adam Ng’imba, alisema kuwa kikao cha usuluhishi baina ya wafugaji hao kimefanyika ili upata suluhu za mgogoro huo na kuwabaini waliofanya mauaji hayo.
CHANZO: NIPASHE