POLISI wa mikoa ya Mwanza, Simiyu na Shinyanga wamefanikiwa kusambatarisha mtandao wa ujambazi kwenye mikoa hiyo baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa wa ujambazi sugu, Njile Samweli (46) mkazi wa kijiji cha Lyoma, Bariadi mkoani Simiyu aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu. Sambamba na kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo wa ujambazi, pia watuhumiwa watano wanashikiliwa, bunduki moja yenye namba PB 3402 aina ya SMG na risasi 331 na kwamba operesheni ya kina inaendelea kwa lengo la kuwakamata watuhumiwa wote pamoja na silaha wanazotumia.
Wakizungumza kwa pamoja Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Valentino Mlowola alisema Januari 5, mwaka huu majira ya saa 7 mchana walimkamata Mabula Lyagwa (36) akiwa na jeraha la risasi kwenye bega lake la kulia baada ya kupokea taarifa kutoka kwa raia wema.

Alisema mtiliwa shaka huyo alipohojiwa alisema kuwa jeraha hilo alipigwa risasi na jambazi mwenzake aitwaye Njile Samweli wakati wakifanya tukio la ujambazi katika kijiji cha Idukilo kata ya Mwadui Luhumbo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Januari 5, saa sita za usiku.


Alisema kutokana na maelezo hayo kikosi cha upelelezi mkoani hapa kiliungana na mikoa mingine na kufanya msako uliofanikiwa kumkamata Njile Samweli ambapo alipohojiwa alikiri kuhusika na matukio mbalimbali ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika mikoa ya Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Tabora na Singida.

Alisema mkoani hapa, mtuhumiwa huyo pamoja na wenzake wamefanya matukio mbalimbali ya uhalifu ambapo Agosti mwaka jana walivamia nyumba ya kulala wageni kwenye kisiwa cha Bulubi, wilayani Ukerewe na kupora Sh milioni 3.5 za wafanyabiashara wa dagaa.


Pia tukio jingine walilifanya Oktoba 2, mwaka jana katika kijiji cha Mahaha wilayani Magu ambapo walivamia maduka na kupora Sh milioni 3 pamoja na pikipiki aina ya Sanlg na kumuua mtu mmoja na kwamba mwezi huo huo walivamia Ngudu ambapo walimjeruhi kwa risasi mtu mmoja na kumpora Sh milioni 2.

Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo alisema mtuhumiwa huyo kwa kushirikiana na wenzake watano wakiwa na silaha SMG No. BP 3402 pamoja na magazine yenye risasi 40 na kiroba kimoja kikiwa na risasi nyingi mali ya Mahenga Nkinda wakiwa ndani ya Hifadhi ya Mawa wakiwinda tembo na faru, ilipofika saa sita usiku, Njile aliamka na kuchukua silaha hiyo na kuwaua wenzake aliokuwa nao kisha kwenda kuichimbia nyumbani kwake.

Alisema Agosti 18, mwaka jana walifanya uvamizi katika duka la mfanyabiashara Igunga na kuua mtu mmoja, kisha aliunda kikosi kingine cha ujambazi ambacho mwezi huo huo walimuua mfanyabiashara wa ng’ombe na kufanikiwa kupora Sh milioni 18 na matukio mengi mawili yaliyofanyika wilayani Maswa ya kuvamia maduka ya wafanyabiashara na kupora.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Justus Gamgisha alisema Januari 5, mwaka huu Njile na kundi lake walifanya uvamizi katika kijiji cha Idukilo ambapo walivamia maduka manne na kupora Sh milioni 3.2 pamoja na simu aina ya Nokia baada ya kufyatua risasi hewani ambapo moja ilimjeruhi jambazi mwenzao Mabula Lyagwa.
 
 
Top