Sherehe za kutahiriwa zimegeuka kuwa msiba, baada ya vijana kumshambulia kwa rungu na kumuua mwenzao wakati wanaserebuka kusherehekea kutoka jandoni, zilizokuwa zinafanyika Bunda mkoani Mara.
Kufuatia mauaji hayo, watu watano wakiwamo watoto watatu wanashikiliwa na polisi wilayani Bunda, kwa tuhuma za kumuua kijana mwenzao kwenye ugomvi wa kugombania msichana uliotokea kwenye sherehe hizo za tohara.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa , Phillipo Kalangi, alisema mauaji hayo yalifanywa usiku wa kuamkia juzi katika kitongoji cha Bunda Stoo, mjini Bunda.

Kalangi alimtaja aliyeuawa kwa kupigwa na rungu kichwani kuwa ni Mandela James (25) mkazi wa mtaa wa Saranga mjini Bunda.

Kwa mujibu wa Kalangi wanaoshikiliwa ni watoto wawili wenye miaka 16 na mmoja mwenye miaka 17 ambao majina yanahifadhiwa kutokana na umri wao kuwa mdogo , Ghati Robhi (26), Justun Robhi (19) ambao wote ni wakazi wa mjini Bunda. Uchunguzi unaendelea kabla ya kuwafikisha mahakamani.

Alisema wakati vijana hao wakiendelea kucheza muziki, wawili kati yao waligombania msichana ndipo mwenzao mmoja akachukua rungu na kumpiga James kichwani na kufa papo hapo.

Kwa mujibu wa mila za Wakurya, vijana huenda porini kwa wiki mbili kutahiriwa na wazee wao na baada ya kupona hurudi nyumbani ambapo sherehe kubwa hufanyika ikihusisha kula nyama za ng'ombe , mbuzi na pombe pamoja na kucheza ngoma mbalimbali likiwamo ritungu.

Na Ahmed Makongo-Mara
 
 
Top