Marehemu Zuhura Juma (31) baada ya kuuliwa na mumewe.

DUNIA inazidi kwenda kubaya! Mwanaume aliyejulikana kwa jina la Maulid Mussa (35), mkazi wa Kijiji cha Igoko wilayani Uyuwi, Tabora anashikiliwa na jeshi la polisi kwa madai ya kumuua mkewe, Zuhura Juma (31) kwa kumchoma visu sehemu mbalimbali za mwili.Tukio hilo la kusikitisha lilitokea saa tisa usiku wa kuamkia Jumatatu ya Januari 12, mwaka huu katika Kijiji cha Usagala Kata ya Magengati Tarafa ya Puge wilayani Nzega, Tabora nyumbani kwa wazazi wa mwanamke huyo.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, Maulid alifikia uamuzi huo mgumu baada ya mkewe kumuuliza habari alizozisikia kuwa aliuza shamba la tumbaku la familia bila yeye kujua hali ambayo haikumpendeza mwanaume huyo.


Bw. Maulid Mussa (35) anayetuhumiwa kumuua mkewe na kujichoma kisu mwenyewe.

Baada ya taarifa hizo mwanahabari wetu alifika kwenye kijiji hicho ili kupata maelezo ya kina kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo.

Kwa mujibu wa shuhuda, siku moja kabla ya tukio, Maulid alimfuata marehemu kwa wazazi wake alipokimbilia baada ya mzozo wa shamba akimtaka arudi nyumbani kuendelea na maisha.

Alipofika, alimkuta mkewe na watoto wao wanne wakila. Alikaribishwa chakula cha mchana, akajumuika.

Siku iliyofuata alimweleza mkewe sababu ya yeye kumfuata ni kutaka arejee nyumbani, lakini mke alikataa kwa vile wazazi wake walikuwa nje ya kijiji hicho.

MUME AWAFUATA WAZAZI
“Baada ya Maulid kupewa maelezo hayo, alichukua uamuzi wa kuwafuata wakwe zake katika Kijiji cha Busondo ambacho ni jirani na kijiji hicho, akawaeleza lengo la safari yake ambapo wakwe hao walimwambia arudi kijijini akawasubiri.”

ALA CHAKULA CHA MWISHO NA FAMILIA
“Maulid alirudi katika kijiji cha wakwe zake. Ilikuwa jioni, akamkuta mkewe ameandaa chakula cha jioni, walikula wote na watoto wao kisha akaaga kwa furaha kwamba anarudi nyumbani kwake,” alisema shuhuda mmoja akiomba jina lake kusitiriwa.

MTOTO WA KAKA WA MAREHEMU ASIMULIA
Shuhuda mwingine wa tukio hilo ni mtoto wa kaka wa marehemu ambaye naye aliomba jina lake lihifadhiwe, yeye alisema:

“Usiku wa tukio nilisikia sauti ya mtoto akilia kuashiria kuna tatizo, nikaamka na kutoka nje ili kujua kuna tatazo gani.
“Nilipofika nje niliona baiskeli ya mume wa marehemu ikiwa imeegeshwa kwenye nyumba aliyolala. Sikuwa na wasiwasi.

“Lakini muda mfupi baada ya kurudi ndani nilisikia sauti ya mwanamke akiomba msaada eneo la nyuma ya nyumba aliyolala marehemu.
Alikuwa akisema, ‘jamani nauawa, naomba mnisaidie nakufa! Nakufa!’ Nikatoka nje na kwenda ilikokuwa ikitokea sauti.
Nilishtuka kumkuta Zuhura amelala chini huku akiwa ametapakaa damu na majeraha mgongoni na shingoni. “Nilipiga kelele kuomba msaada, watu wakaja. Ndipo tukaanza kumfuatilia Maulid kwani niliwaambia niliiona baiskeli yake nje ya nyumba.

“Tulimkuta Maulidi kichakani naye akiwa ametapakaa damu. Kumbe alijaribu kujichinja mwenyewe shingoni kwa lengo la kujimaliza baada ya zoezi la kujiua kwa kunywa sumu kushindikana ambapo alitapika.”

BABA WA MAREHEMU
Naye baba wa marehemu Zuhura, Juma Ramadhani alipozungumza na mwandishi wa habari hizi kuhusu mauaji ya mwanaye alisema:


Marehemu Zuhura Juma enzi za uhai wake.

“Kusema ukweli maumivu niliyoyapata kwa kuuawa mtoto wangu tena kikatili vile siwezi kuyatolea mfano. Mimi nachukulia mauaji haya kama kuidhalilisha familia yangu. Naiomba serikali itende haki kwa kutoa hukumu na adhabu kali kwa Maulid ili iwe fundisho kwa wanaume wenye tabia ya kufanya ukatili kwa wake zao.”

MWENYEKITI WA KIJIJI
Mwenyekiti wa Kijiji cha Usagali, Ally Said Mlenda alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na aliyapokea kwa masikitiko makubwa.

HALI YA MTUHUMIWA
Wakati habari zinakwenda mitamboni, mtuhumiwa huyo yuko chini ya ulinzi katika Kituo cha Polisi Nzega akisubiri kupandishwa mahakamani kwa madai ya kumuua mkewe.

~Credit GPL
 
 
Top