Mary Naali wa mbele akiwajibika.

Mshindi wa 2010 wa mbio fupi (half marathon) za Vienna, Mary Naali ni miongoni mwa wanariadha maarufu nchini Tanzania waliothibitisha kushiriki mbio maarufu za Kilimanjaro Marathon zitakazofanyika mapema mwezi ujao mkoani Kilimanjaro, Kaskazini mwa Tanzania.Akiwa na rekodi nyingine ya kushinda mbio za kimataifa za Bucharest zilizofanyika kati kati ya mwaka 2013 kwa muda wa 1:16:32, Naali atapata upinzani mkubwa kutoka kwa wakimbiaji hodari wa Kenya kama vile Jacqueline Sakilu, aliyeshinda half marathon ya Kilimanjaro Marathon mwaka jana.

Mkurugenzi wa mbio za Kilimanjaro Marathon, John Bayo amesema wakimbiaji wengi wa Tanzania na wa kimataifa wameonesha nia ya kushiriki mbio hizo, zinazotambuliwa na Shirikisho la riadha duniani (IAAF).

Fabian Joseph, Mtanzania aliyeshinda half marathon Edmonton, Canada mwaka 2005, ni miongoni mwa wakimbiaji wengine watakaoshiriki.

Mbio hizo zitafanyika March 1 na moja ya malengo yake, mbali ya kuwaandaa wakimbiaji kwa ajili ya michuano ya kimataifa, ni kuendeleza utalii wa ndani.

Zaidi ya wakimbiaji 200 kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na kwingineko hupata fursa ya kuuona Mlima Kilimanjaro, ambao ndio mrefu kuliko milima yote barani Afrika wakati wa mbio hizo.

Kenya, moja ya nchi zinazoongoza katika riadha barani Afrika, imeshinda medali nyingi tangu michuano hiyo ilipoanza na washindi wa mwaka jana wa mbio ndefu (full marathon) wote walitoka Kenya. 
 
 
Top