HATIMAYE Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw.Kabwe Zitto (PICHANI) amekubali yaishe na kuamua kuaga wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, Watanzania, Wabunge wenzake na Wajumbe wa Kamati wa Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kabla ya kutangaza kuachia Ubunge wake.
Zitto alichukua hatua hiyo inayoingia katika historia yake na ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akisema ameondolewa na “mfumo ambao unatukuza Parties’ Power (nguvu za chama) badala ya People’s Power (nguvu ya umma).”

*Historia ya sakata 

Akielezea namna alivyofikia uamuzi huo, Zitto alisema kwa muda mrefu pamekuwa na msuguano wa kiuongozi kati yake na viongozi wa ndani ya CHADEMA, uliosababishwa na tofauti za kimtazamo juu ya tafsiri pana ya demokrasia ndani ya chama. “Hatimaye tofauti hizi zilisababisha Novemba 2013, Kamati Kuu ya Chadema ikanivua nafasi zangu zote za uongozi nilizokuwa nazo.

Sikuridhika na uamuzi huo na hivyo nikaonesha kusudio la kukata rufaa katika Baraza Kuu la chama chetu kama taratibu za kikatiba za chama chetu zinavyotaka.

“Bahati mbaya ofisi ya Katibu Mkuu haikunipa fursa hiyo, na huo ndio ukawa msingi wa mimi kufungua kesi mahakamani kuweka pingamizi la Kikao cha Kamati Kuu kujadili hatima ya uanachama wangu hadi pale ofisi ya Katibu Mkuu itakaponipa fursa ya kukata rufaa katika vikao vya chama,” alisema.

Alisema hatimaye Mahakama Kuu imetoa hukumu yake Machi 10, mwaka huu 2015 na katika hukumu hiyo, ameshindwa kwa sababu za kiufundi kwa maelezo kwamba pingamizi lake liliwasilishwa kimakosa.

“Pamoja na kwamba hatukuridhika na jinsi kesi hii ilivyoamuliwa pamoja na maudhui ya hukumu yenyewe, ninaheshimu uamuzi wa mahakama na sina mpango wa kukata rufaa,” alisema.


Alivyofitiniwa “Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida na kwa mujibu wa Katiba ya chama chetu, ilitarajiwa kwamba baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu, Kamati Kuu ingekaa na kunipa rasmi mashitaka yangu yanayohusu uanachama wangu, mimi kuitwa kujieleza na hatimaye Kamati Kuu kutoa uamuzi wake. “Hata hivyo,mara baada ya hukumu ya Mahakama Kuu, dunia nzima ilitangaziwa na Mwanasheria wetu Mkuu (Tundu Lisu), kwa niaba ya chama, kwamba mimi nimeshafukuzwa na sio mwanachama tena wa Chadema,” alisema.

Alifafanua kwamba viongozi wake wametoa matamko mbalimbali yote yakionesha kwamba hatakiwi tena katika chama hicho, ingawa hadi jana alipokuwa akizungumza hakuwahi kukabidhiwa barua yoyote iiliyotaarifu kufukuzwa kwake katika chama.

“Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo ya hapo juu, ni wazi kwamba uanachama wangu wa kisiasa ndani ya Chadema umeshaondolewa. Ninaweza kuendelea kupigania uanachama wangu kisheria na kwa kweli nina sababu na misingi yote kubaki na uanachama wangu kisheria. “Lakini mimi ni mwanasiasa. Sikuja hapa bungeni kwa sababu ya kushinda kesi mahakamani. Nilichaguliwa na wananchi wa Kigoma Kaskazini na ninatambua kwamba huwezi kuwa mbunge bila udhamini wa chama cha siasa. Huu ndio utaratibu wa kisheria tuliojiwekea,” alisema.

Anavyoondoka Zitto 

Alisema kutokana na maelezo yake, anaomba kumtaarifu Spika Anne Makinda na Bunge kwamba hana mpango wa kuendelea kupigania uanachama wake wa Chadema katika viunga vya mahakama. “Kwa hiyo ninatangaza rasmi leo kwamba taratibu za kikatiba zitakapokamilika tu, nitaachia uanachama wa Chadema, chama nilichokipenda sana kwa sababu ya kuendelea kukua kwa tofauti za kiitikadi, kimtazamo na hata kibinafsi kati yangu na viongozi katika chama changu.

“Ni matumaini yangu kwamba Bunge lako Tukufu halitaruhusu mfumo huu unaoruhusu vyama vya siasa kupora mamlaka ya wananchi uendelee.

Ni Bunge lako pekee lenye uwezo wa kukomesha mfumo ambao unatukuza Parties’ Power, badala ya People’s Power,” alihitimisha. 

Ushauri Chadema 

Akitoa ushauri kwa Chadema, chama alichosema anakipenda sana, Zitto alisema inawezekana wasiweze kuelewana katika masuala ya uongozi, misingi na itikadi, lakini anaamini wanapaswa kuelewana na kukubaliana katika dhamira kubwa ya kuijenga nchi kuwa Taifa linalojitegemea na lisilo na aina yoyote ya ubaguzi.


“Ni matumaini yangu kuwa tutakuwa bega kwa bega katika harakati hizi katika siku zijazo. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo.


Nafasi hii ya kihistoria tuliyopewa haihitaji siasa za ubinafsi na unafsi! Uzalendo wetu utapimwa kwa uwezo wetu wa kuweka tofauti zetu binafsi pembeni kwa lengo lililo kubwa zaidi yetu,” alishauri. 


Mafao Awali akizungumza na gazeti hili kuhusu mafao yake kabla ya kuaga, Zitto alisema suala la msingi kwake ni kuingia mstuni kufanya siasa na wala hajali kupoteza kiinua mgongo chake cha ubunge. “Mimi sijali nitakosa nini maana hata kiinua mgongo chenyewe sijui ni kiasi gani, nina miaka mingi nimekuwa sichukui posho yangu ya ubunge sembuse hicho kiinua mgongo? Alisema Zitto. 


Hata hivyo, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema kwamba mbunge anayeacha ubunge wake, inawezekana akalipwa mafao yake au asilipwe kulingana mazingira yake ya kuacha ubunge. 


Alifafanua kuwa kama mbunge ameacha ubunge kwa kulazimishwa na chama chake, atalipwa stahili zake lakini kama ameacha ubunge kwa utashi wake mwenyewe halipwi. “Huwezi kuacha ubunge kwa hiari halafu udai malipo, hapo umeacha kazi kwa hiari huwezi kulipwa, lakini kwa suala la Zitto ambaye sijapata taarifa kama kaachia ubunge, yeye amelazimishwa na chama chake.


“Hivyo mazingira hayo atalipwa kiinua mgongo maana jambo hilo linamgusa binafsi pamoja na jamii kwa ujumla,” alisema Joel . 


Maandalizi ACT .


Taarifa zinazozungumzwa, zilidai kuwa wakati Zitto akitangaza uamuzi huo, ndani ya chama cha ACT kulikuwa na maandalizi na vikao vilivyokuwa vikiendelea, kwa ajili ya kumpokea mbunge huyo. 


Kwa mujibu wa madai ya mtoa habari wetu, ACT inajiandaa kumpokea Zitto kesho na tayari ameshaandaliwa moja ya vyeo vya juu vya chama hicho, lakini si Uenyekiti.HOTUBA YA ZITTO ALIYOTAKA KUITOA BUNGENI JANA MARCH 20,2015 BOFYA HAPA KUISOMA


Source:-Habari Leo.



 
Top