Viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi, UKAWA.

Gazeti la Mtanzania la jana March 19,2015, limeripoti taarifa kuwa kamati maalumu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), imekamilisha kazi ya ugawaji wa majimbo 211 ambayo ni sawa na asilimia 88 kati ya majimbo yote 239.
Wakati hayo yakiendelea, kamati hiyo imeshindwa kuafikiana katika majimbo 28 ambayo yanasubiri uamuzi wa Wenyeviti wa Vyama vinavyounda UKAWA, ambao watamaliza kiporo hicho mwezi huu.

Hatua hiyo imekuja baada ya viongozi wa juu wa umoja huo, kutangaza mkakati wa kusimamisha mgombea mmoja wa Urais na kuachiana majimbo ya uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba,Mwaka huu 2015.

UKAWA ni umoja ulioanzishwa Februari mwaka jana 2014 wakati wa Bunge Maalumu la Katiba, ukiundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, CHADEMA, CUF na NLD.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kamati hiyo maalumu ya UKAWA, kiliiambia gazeti hilo March 18,2015, kuwa kwa muda wa wiki moja sasa, kamati hiyo imekamilisha kazi hiyo kwa kiwango kikubwa jambo ambalo limeelezwa linaweza kutoa upinzani mkali kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu.


“Kamati ilitafiti namna gani bora ya kuachiana Madiwani, Wabunge naRais ili tusimamishe mgombea mmoja katika kila eneo, lakini tulivutana kwani kila upande uliangalia masilahi yake, ingawa katika suala linaloitwa laushirikiano ni lazima ukubali kupoteza sehemu na ninaamini UKAWA sasa itakuwa imara zaidi,” kilisema chanzo cha habari.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, mgawanyo wa majimbo kwa Mkoa wa Dar es Salaam umeangalia vigezo vya kukubalika kwa mtu pamoja na yalipo makao makuu ya chama.

Kutokana na hali hiyo, CHADEMA imekubaliwa itasimamisha wagombea katika majimbo ya Ubungo, Kawe, Kinondoni na Ukonga huku CUF ikiachiwa majimbo ya Segerea, Temeke na Kigamboni na NCCR-Mageuzi ikipewaIlala.

Mkoa wa Kilimanjaro majimbo ambayo yamepitishwa uamuzi kuachiwa CHADEMA kuwa ni Moshi Mjini, Moshi Vijijini, Rombo, Same Mashariki, Same Magharibi, Hai na Siha, huku NCCR-Mageuzi ikiachiwaVunjo na Mwanga.

Kigoma NCCR-Mageuzi imeachiwa kusimamisha wagombea katika majimbo sita ya Kasulu Mjini, Kasulu Vijijini, Buhigwe, Muhambwe, Buyungu naKigoma Kusini na CHADEMA ikibaki na Kigoma Mjini na Kigoma Kaskazini.

Katika majimbo 28 ambayo ni tata, kamati hiyo maalumu imeitaka kamati ya kitaifa ya UKAWA kuwezesha kukubaliana kwa baadhi ya vyama ambapo katika Jimbo la Mtwara Mjini NCCR-Mageuzi na CUF vinatakiwa kukaa na kukubaliana kuachiana.

Mbali na hilo pia katika Jimbo la Babati Vijijini, CHADEMA na NCCR-Mageuzi wanatakiwa kukaa na kukubaliana namna ya kuachiana.

Aidha, kamati hiyo maalumu ya wataalamu wa Ukawa imeshauri kuwa kwa majimbo yanayoongozwa na wabunge kutoka upinzani kwa sasa yatabaki kwa vyama husika bila vyama vinavyounda Ukawa kuteua wagombea wengine.

Chanzo : MTANZANIA.

 
Top